18th January 2013
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe |
Kutolewa kwa maamuzi hayo kumefuatia taratibu za kupitia mapendekezo yaliyotolewa na bodi ya mamlaka hiyo kwa Wizara ya Uchukuzi kukamilika.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo NIPASHE imezipata kutoka vyanzo vya ndani ya TPA na Bodi ya TPA, kilichobakia ni kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua zitakazochukuliwa.
“Hivi sasa mapendekezo yaliyotolewa bodi, wizara imeshamaliza kuyapitia na kutoa uamuzi wa hatua za kuwachukuliwa waliosimaishwa,” alisema ofisa mmoja kutoka TPA ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hakuna haja kwa vyombo vya habari kuwa na ‘presha’ kwani muda ukifika uamuzi utakaokuwa umetolewa dhidi ya vigogo hao wa TPA taarifa itatolewa.
Jumatatu wiki hii, Dk. Mwakyembe alithibitisha kupokea ripoti ya mapendekeo yaliyotolewa na Bodi ya TPA dhidi ya viongozi waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi kwa ajili ya maamuzi. Wiki iliyopita gazeti hili lilidokezwa kuwa Bodi hiyo imemaliza kuwahoji viongozi hao na kuwasilisha mapendekezo kwa Waziri.
Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria za Bandari, maamuzi kuhusu hatma ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraem Mgawe, ambaye ni miongoni mwa vigogo sita waliosimamishwa kazi, hayaihusu bodi bali Waziri.
Taarifa zilieleza kuwa bodi imemaliza kumhoji Mgawe na kupokea
utetezi wake na kwamba taarifa ya uchunguzi dhidi yake iliwasilishwa mezani kwa Waziri Mwakyembe tangu wiki iliyopita.
Agosti mwaka jana, Dk. Mwakyembe alimsimamisha kazi Mgawe na maofisa wengine sita kufuatia tuhuma za ufisadi katika mamlaka hiyo.
Wengine waliosimamishwa ni manaibu wakurugenzi wawili wa TPA, Julius Mfuko (Maendeleo ya Miundombinu); Hamad Kashuma (Huduma); Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng’amilo na mameneja wawili wa Bohari ya Mafuta Kurasini Oil Jetty (KOJ) pamoja na mhandisi wa bohari hiyo.
Hatua ya bodi kuwahoji inafuatia kukamilika kwa taarifa ya uchunguzi dhidi ya menejimenti ya TPA. Waziri Mwakyembe ndiye aliyeagiza uchunguzi dhidi yao ufanyike Agosti mwaka jana.
Dk. Mwakyembe alisema vigogo hao walisimamishwa kwa muda ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazoikabili menejimenti ya TPA zikiwamo wizi wa makontena, wizi wa mafuta, udokozi wa mizigo na rushwa katika utoaji wa huduma.
No comments:
Post a Comment