Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Februari
14, 2013 ameungana na mamia kwa mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki, Jimbo la
Moshi na kutoka sehemu nyingine nchini, kumzika Askofu Mstahivu (Bishop
Emeritus) Amedeus Peter Msarikie.
Rais Kikwete
amewasili kwenye Kanisa Kuu la Kristo Mfalme mjini Moshi kiasi cha saa sita na
dakika tano mchana kuungana na marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin
Mkapa na mamia kwa mamia wananchi kwa ajili ya mazishi ya Askofu Msarikie
ambaye alifariki dunia Alhamisi iliyopita, Februari 7, 2013 kwa ugonjwa wa
saratani katika hospitali moja mjini Nairobi, Kenya.
Mara baada ya
kuwasili, Rais Kikwete ametia saini kwenye kitabu cha maombolezo na ikaanza
ibada ya mazishi ilivyohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi wakiwamo
maaskofu zaidi ya 20 kutoka majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini.
Mwili wa Marehemu
Msarikie uliteremshwa kaburini kiasi cha saa saba na dakika 35 ndani ya Kanisa hilo na Rais Kikwete akaweka udogo kwenye kaburi na
baadaye shada la maua.
Akizungumza kwenye
mazishi hayo, Rais Kikwete amemwelezea Askofu Msarikie ambaye alikuwa Askofu wa
Jimbo la Moshi kwa miaka 26 kama “kiongozi
shupavu wa kiroho ambaye aliwalea vyema kondoo wa bwana. Lakini pia alikuwa
kiongozi hodari kwa maendeleo ya jamii yaliyowanufaisha waumini wake na hata
wale wa madhehebu na dini nyingine.”
Amesisitiza Rais
Kikwete: “Kwa kweli sote tumepoteza mtu muhimu. Tunamfahamu marehemu Baba
Askofu Msarikie kwa mema mengi aliyowatendea watu wa jimbo lake, ya kiroho na
ya maendeleo. Mimi binafsi, wana-moshi na Watanzania kwa ujumla tutamkumbuka na
kumuenzi Baba Askofu Msarikie kwa mema mengi aliyowafanya wanadamu wenzake na
nchi yetu.”
Rais Dkt.Jakaya
Mrisho Kikwete akitoa heshima za Mwisho mbele ya jeneza la Askofu Mtsaafu jimbo
Katoliki la Moshi Marehemu Mhashamu Amedeus Msarikie wakati wa misa ya Mazishi
iliyofanyika katika kanisa na Kristu Mfalme, mjini Moshi leo.
Rais Dkt.Jakaya
Mrisho Kikwete akiweka udongo katika kaburi la Askofu Mstaafu Jimbo katoliki la
Moshi,Marehemu Mhashamu Amedeus Msarikie wakati wa ibada ya mazishi
Iliyofanyika katika Kanisa la Kristu Mfalme mjni Moshi leo.
Rais Dkt.Jakaya
Mrisho Kikwete akiweka shada la maua
katika kaburi la Askofu Mstaafu jimbo Katoloki la Moshi Marehemu Mhashamu
Amedeus Msarikie wakati wa ibada ya mazishi Iliyofanyika katika Kanisa la
Kristu Mfalme mjni Moshi leo. Picha na Freddy Maro wa Ikulu
No comments:
Post a Comment