Saturday, January 26, 2013

JAPAN YATOA MABILIONI UJENZI WA BARABARA ZA JUU DAR.

Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa
Na Beatrice Shayo;

Ujenzi wa barabara za juu nchini uko mbioni baada ya Serikali ya Japani  kuisaidia Serikali ya Tanzania Sh. bilioni 28.2 kwa ajili ya kufadhili miradi mitatu, ikiwemo ya ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Tazara, Nyerere na Nelson Mandela jijini Dar es Salaam.

Makubaliano ya mkataba huo, yalisainiwa jana jijini Dar es Salaam kati ya Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada kwa niaba ya Serikali ya Japan.

Akiongea mara baada ya kusaini mkataba huo, Mgimwa alisema Serikali ya Japani imekubali kusaidia miradi hiyo mitatu, wa kwanza ukiwa ni ujenzi wa barabara ya juu katika eneo la Tazara na michoro kwa ajili ya ujenzi huo utakaogharimu Sh bilioni 1.1 ipo tayari.

Alisema ujenzi wa barabara hizo za juu utapunguza foleni pamoja na kuboresha usafirishaji jijini na  kusaidia kuinua uchumi na kuimarisha shughuli za kibiashara.

Alisema mradi wa pili ni upanuzi wa barabara ya Kilwa pamoja na eneo la Bandari ili kutatua msongamano wa magari ambapo ujenzi huo utagharimu Sh. bilioni 20.

Alisema shughuli za usafiri zina umuhimu mkubwa katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kupunguza umasikini.

Dk. Mgimwa alisema mradi wa tatu utakaogharimu Sh bilioni 6 utatumika kwa ajili ya usalama wa chakula nchini ili kutatua tatizo la uhaba wa chakula na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Alisema serikali ya Japan ipo tayari kusaidia mpango wa Kilimo Kwanza kupitia mradi huo wa usalama wa chakula kwa wakulima wadogo.

Alisema fedha hizo za usalama wa chakula nchini zitakapotolewa, serikali itatoa kipaumbele kwa mikoa yenye uhaba wa chakula na tatizo la njaa.

Kwa upande wake Balozi Okada alisema mradi huo wa barabara mbili za juu utakapokamilika utarahisisha usafiri kutoka katikati  ya mji hadi Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo awali ulitumiwa kwa dakika 37 na kwamba itakapokamilika barabara hiyo itatumia muda wa dakika 25. Alisema anaamini ujenzi wa miundombinu hiyo utasaidia kuinua uchumi na kupunguza umasikini kwa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger