By Khatib Suleiman
WIZARA ya Biashara, Viwanda na Masoko imesema imetumia jumla ya Sh milioni 202 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitano vya kununua karafuu kutoka kwa wakulima kisiwani Pemba.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Thuwaiba Edikton Kisassi wakati akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, Salim Abdalla Hamad(CUF) aliyetaka kujua mikakati ya Shirika la Taifa la Biashara(ZSTC) katika kujenga vituo vyenye hadhi ya kununua karafuu Pemba.
Kisassi alivitaja vituo vilivyojengwa kwa ajili ya kununua karafuu na kuwapunguzia mwendo mrefu wakulima ni Mkanyageni, Mzambarau takao, Kinyasini pamoja na Raha na Chonga.
Alisema ZSTC imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima ikiwemo kuwapunguzia mwendo mrefu wa kupeleka Karafuu zao kwa ajili ya manunuzi.
Aidha Kisassi alisema vipo jumla ya vituo 36 vya kununua Karafuu Unguja na Pemba.
“Tunaweza kuongeza vituo vya kununua karafuu kama mahitaji na mavuno ya msimu wa Karafuu yatakuwa makubwa,” alisema.
Msimu wa karafuu wa mvua za vuli unaendelea katika kisiwa cha Pemba ambapo ZSTC inaendelea na utaratibu wa kununua karafuu kutoka kwa wakulima.
ZSTC katika msimu wa mavuno ya karafuu mwaka jana imenunua zaidi ya karafuu tani 4,822.8 zenye thamani ya Sh bilioni 72.1.
No comments:
Post a Comment