WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amependekeza katika Katiba mpya ijayo, madaraka ya Rais yapunguzwe hasa katika shughuli za uteuzi wa viongozi.
Akizungumza jana baada ya kutoa maoni mbele ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Pinda alisema muda aliokaa madarakani na Rais Jakaya Kikwete, ameona ana mambo mengi na ndiyo maana anapendekeza si lazima kila jambo liende kwake.
“Ni vema machache yabaki kwake. Kwa mfano uteuzi wa nafasi mbalimbali vipewe vyombo vya kufanya uteuzi huo,” alisema bila kufafanua nafasi ambazo Rais anatakiwa kuacha kuteua. Kuhusu nafasi ya Waziri Mkuu, alisema hiyo ni ya utendaji na kwa sasa Waziri Mkuu lazima awe mbunge na kutokana na hali hiyo, anapendekeza itazamwe vizuri.
Alifafanua kuwa Waziri Mkuu atajikuta akilazimika kuangalia zaidi Serikali huku jimbo analowakilisha likilala kwa kukosa usimamizi mzuri.
Kutokana na hali hiyo, alipendekeza mawaziri wasitokane na wabunge, ili wafanye kazi vizuri ya kusimamia majimbo yao wakisaidiana na wananchi. Uhuru wa Bunge, Mahakama Alisema Bunge na Mahakama ni vyombo muhimu vinavyostahili kupewa nafasi ya kutosha.
Alizungumzia mifuko iliyoundwa ya Bunge na Mahakama na kutaka itambuliwe kikatiba na Katiba ielekeze ni namna gani itumike. Kuhusu kinga ya mbunge, alisema ni vizuri itamkwe kwenye Katiba kuwa mbunge ana kinga, lakini ibaki bungeni tu si azungumze nje na kinga ya Bunge iendelee kumlinda.
Akizungumzia Muungano, Pinda alisema tangu azaliwe hadi anapata akili mwaka 1964, alikuta Muungano na ndicho kitu pekee anachoweza kukisemea vizuri kwa kuwa umejenga udugu, muungano na ukaribu.
“Hapakuwa na huyu ni mgeni, au huyu ametoka huku au kule,” alisema akizungumzia Muungano wa Serikali mbili ulivyo. Alikiri kuwa kuna kero nyingi za Muungano na kupendekeza kuwa dawa ya kero hizo si kuua Muungano, bali kitafutwe chombo kitakachoshughulikia matatizo.
Alipendekeza Serikali zibaki mbili lakini iundwe tume ya kushughulikia matatizo yaliyopo. Pia akapendekeza kuundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa Tanzania Bara kama ilivyo Zanzibar na vyama vyote vipate ushiriki. Mafuta, gesi Akizungumzia rasilimali za Taifa za mafuta na gesi, Pinda alisema haoni shida mafuta kuchimbwa Zanzibar na kusafirishwa Bara au kuchimbwa Bara na kusafirishwa Zanzibar kwa kuwa atavuka tu kununua na kurudi.
No comments:
Post a Comment