Friday, January 25, 2013

RUBADA YAANZISHA MKAKATI KUENDELEZA KILIMO NYANDA ZA KUSINI

MAMLAKA ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) imeandaa mkakati wa kuanzisha kambi za vijana ikiwa ni njia mojawapo ya kuwahamasisha kujishughulisha katika kilimo kupitia Mpango wa Uendelezaji wa Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT)

RUBADA inataka kuwaunganisha vijana walio katika vijiji mbalimbali wilayani humo, ili waweze kuingia katika kilimo na kuwaondoa na fikra potofu za kukaa vijiweni bila sababu za msingi.

Mkurugenzi Mkuu wa RUBADA, Aloyce Masanja, alisema hayo wakati wa semina ya kuwajengea uwezo watendaji wa ngazi ya vijiji hadi wilaya wilayani Ludewa, Njombe juu ya mpango mzima SAGCOT na Kilimo Kwanza.

Alisema vijana wengi nchini wamekuwa wapigadebe wakubwa katika siasa bila kujishughulisha na shughuli za maendeleo, hivyo wao kama mamlaka wana wajibu wa kuwajenga kifikra ili waweze kufanya kazi za kilimo na kuweza kuimarisha uchumi wao na familia zao.

Akitolea mfano nchi ya Korea, alisisitiza kuwa Wakorea wamepiga hatua kubwa kwa kujikita katika sekta ya kilimo, hivyo ni vema Watanzania hasa vijana wakaelekeza nguvu zao katika kilimo, ili kuweza kuinua uchumi wa nchi na kuimarisha ustawi wa jamii.

Aliongeza kuwa, Wilaya ya Ludewa ina fursa nyingi za kilimo, hivyo ni wajibu wa kila mwana-Ludewa kujivunia hali hiyo ili waweze kuitumia kwa uhakika katika kukuza kilimo hasa kilimo cha biashara ili kuongeza kipato.

Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Fidelis Lumato, alisema wilaya hiyo ina eneo lenye ukubwa wa hekta 839,700 na kati ya hizo 207,200 ni eneo lenye maji, hivyo ni ukanda unaofaa kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji.

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger