KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amewaachia neema
wakazi wa wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, baada ya kuchangisha zaidi ya sh.
milioni 18 za ujenzi wa wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya hiyo, kwenye
mkutano wake wa hadhara uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Ushirika mjini
wilayani hapa.
Katika mkutano huo ambao ulikuwa unahitisha ziaya ya siku
mbili wilayani humo, ikiwa ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya miaka 36 ya
CCM, ambazo kilele chake ni Jumapili hii kwenye Uwanja wa Lake
Tanganyika mjini Kigoma, Kinana alianza harambee hiyo kwa
kuchangia sh. milioni 10.
Baada ya mchango huo aliwachagiza viongozi wote waliokuwa
jukwaa nao wakatoa michango yao,
wakiwemo Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi CCM, Alhaj Abdallah Bulembo ambaye
alitoa milioni 2.3 na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma, Dk. Amani Kaborou
aliyechangia sh. milioni moja.
Pamoja na michango hiyo, Kinana alitoa ahadi kwamba baada ya
ujenzi wa wodi kukamilika Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete atatoa vifaa
vyote vinavyotakiwa kuwemo ikiwa ni pamoja na vitanda vya kujifungulia kina
mama.
"Ndugu wananchi kwa niaba ya Mwenyekiti wetu wa Chama
Rais Jakaya Kikwete naomba kuahidi kwa niaba yake kwamba, baada ya ujenzi wa
wodi kukamilika atatoa vifaa vyote vihavyohitajika kuifanya wodi itoe huduma
bora, na kwa hili nina uhakika hataniangusha atatoa", alisema Kinana.
Uchangishaji huo ulifuatiwa na malamiko ya wananchi na
baadjhi ya viongozi kwenye mkutano huo uliofurika maelfu ya watu, ambao
walisema, hadi sasa hospitali ya wilaya ya Kibondo ina chumba kimoja tu cha
wodi ya wazazi ambacho kakikidhi mahitaji kiasi kwamba baadhi ya wanaokwenda
kujifungua wanalala chini kwa kukosa vitanda.
"Ndugu Katibu Mkuu wa CCM, nikiwa kama mama na Mwenyekiti wa Umoja wa
Wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya
Kibondo na diwani wa Kata ya Kibondo
mjini naomba kuweka bayana kwamba hapa tuna tatizo kubwa wa wodi ya kinana
mama, tuna chumba kimoja tu ambacho hakitoshi kiasi kwamba baadhi ya wanaenda
kujifungua hulala chini", alisema Joyce Chuma.
Mapema kabla ya harambee hiyo, Kinana alifanya harambee
nyingine kwa ajili ya kusaidia kwenda shule za sekondari watoto wanaofaulu huku
wakiwa walezi au wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha.
Ombi la kufanyika harambee hiyo lilitolewa na Mkuu wa wilaya
ya Kibondo, Venance Mwamoto ambaye alisema kwenye mkutano huo kwamba kuna kiasi
cha watoto kumi ambao wameshindwa kwenda shule kutokana na wazazi au walezi wao
kutokuwa na uwezo.
Ili kuchagiza uchangiaji
huo, Mwamoto alijitolea mbuzi aliyeletwa mkutanoni Kinana akampiga mnada ambapo
kwanza alimnunua mbuzi huyo kwa sh. milioni 3 na kuwapatia wasanii wa muziki
wabongo Fleva ambao walitumbuiza kwenye mkutano huo.
Pamoja na Kinana wachangiaji wengine walijitokeza na hadi
mwisho wa mnada zilipatikana sh. milioni 6.6.
Ili kufanya uchangiaji huo
uwe endelevu Kinana aliahidi kutoa sh. milioni tatu kila mwaka endapo Mkuu huyo
wa wilaya atafungua mfuko maalum wa kuwsomesha watoto ambao wamefaulu lakini
wazazi au walezi wao hawana uwezo.
Akizungumzia kero ya muda mrefu ya Barabara ya
Nyakanazi-Kigoma kupitia wilaya za Kibondo na Kasulu mkoani Kigoma, Kinana alisema,
barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami kama
ilivyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete wakatin wa kampeni.
"Wananchi ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami
lazima utafanyika kwa sababu ahadi hii ipo katika ilani ya CCM na ni ahadi ya
Rais Jakaya Kikwete hivyo msiwe na shaka na hili, nitamkumbusha Rais wetu,
Jakaya Kikwete na bila shaka atalipa mkipaumbele swala hili", alisema
Kinana.
Rais Jakaya Kikwete alitaraajiwa kuwasili mjini Kigoma leo
Februari 2, 2013 kwa ajili ya sherehe za miaka 36 ya CCM zitakazofanyika
Jumapili hii kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.
No comments:
Post a Comment