SERIKALI kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imefunga jumla ya transfoma mpya 15 katika vituo vya Buguruni, City Center, Kariakoo, Kipawa, Mbagala, Mbezi, Oysterbay na Ubungo ili kuboresha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa bungeni mjini hapa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akisoma hotuba ya bajeti kwa Wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.
Waziri Muhongo alisema vile vile ufungaji wa transfoma mpya katika vituo vya Bahari Beach, Gongo la Mboto, Kigamboni na Kunduchi upo katika hatua za mwisho za utekelezaji na kwamba mradi huo utakamilika mwaka 2014/2015 na kugharimu Sh bilioni 120.
Alisema ufungaji wa transfoma hizo utaongeza kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa umeme katika Jiji la Dar es Salaam na kuongeza mapato yatakayotokana na uzalishaji katika maeneo mbalimbali.
“Kazi ya kubadilisha nyaya zenye ukubwa wa milimita 150 na kuweka zenye ukubwa wa milimita 432 pamoja na kubadilisha nguzo zilizooza kwenye njia ya umeme ya kilovoti 33 Ilala – Kurasini imekamilika kwa asilimia 99,” alisema Waziri Muhongo.
Waziri alisema kazi iliyobaki ni kukarabati maungio yote tangu mwanzo wa njia hadi mwisho. Alisema njia hiyo ya umeme inakatika mara kwa mara na kusababisha wateja wa maeneo ya Kigamboni, Kurasini, Mbagala na Mkuranga kukosa umeme.
“Baada ya ukarabati kukamilika, wateja wa maeneo hayo sasa wanapata umeme wa uhakika tofauti na ilivyokuwa kabla,” alisema Waziri.
Alisema kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kumpata mkandarasi ambaye ni Kampuni ya M/S ELTEL Group OY kutoka Finland kwa ajili ya kutekeleza mradi wa huduma za umeme jijini Dar es Salaam.
Alisema mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Finland kwa gharama ya Euro milioni 25 sawa na Sh bilioni 57.50 na serikali itachangia Euro milioni 1.50 sawa na Sh bilioni 3.45 .
No comments:
Post a Comment