Monday, June 24, 2013

SERIKALI 3, MTIHANI MKUBWA -UVCCM

Mwenyekiti wa UVCCM, Taifa, Sadifa Juma Khamis
Mwenyekiti wa UVCCM, Taifa, Sadifa Juma Khamis

 

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Taifa, Sadifa Juma Khamis amesema haafiki kuwepo kwa serikali tatu kwa kuwa upo uwezekano mkubwa wa muungano uliopo kuvunjika iwapo Katiba itahalalisha mfumo huo.

Hamis ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Donge , aliyasema hayo jana  kwenye mahafali ya wanafunzi wa vyuo vikuu Mkoa wa Kilimanjaro, ambao ni makada wa chama hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa CCM mkoani hapa Juni 23,2013.

“Tanzania yetu haijafikia uwezo wa kuendesha serikali tatu, tusijidanganye kwani mfumo huo tayari utavunja kabisa muungano uliopo na kila mtu kuwa na nchi yake…mimi na Jumuiya yangu (UVCCM) siafiki kuwapo kwa serikali tatu hata kidogo kwa sababu ni mzigo kwa wananchi” alisema Khamis.

Alisema kutokana na uchumi wa nchi kuwa mdogo, haitawezekana kuhudumia serikali tatu kwani badala ya wananchi kuletewa maendeleo, fedha hizo zitatumika kuendesha masuala ya serikali hizo.

Hamisi alisema muungano uliopo ndio njia sahihi ya kutatua matatizo ya Watanzania pamoja na kudumisha amani, lakini unaweza kuvunjika endapo wananchi hawatafikiria kwa makini juu ya serikali tatu ambazo zitatumia rasilimali zao kuendesha shughuli za kawaida badala ya maendeleo.

Alisema serikali tatu itasababisha rais watatu ambao katika kuchangia muungano kila mtu atavutia kwake, wapo wenye rasilimali nyingi na wengine chache hivyo itasababisha kila mmoja kujitegemea na Rais wa Muungano hatakuwa na nguvu tena.

Mapendekezo yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ni kwamba Jamhuri ya Muungano itakuwa na muundo wa shirikisho lenye serikali tatu ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania Bara.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya utekelezaji kwa mambo yote yaliyoorodheshwa kuwa Mambo ya Muungano, na wakati inapotekeleza majukumu yake, itazingatia mamlaka yake iliyopewa chini ya Katiba.

Washirika wa Muungano watakuwa na hadhi na haki sawa ndani ya Jamhuri ya Muungano na watatekeleza majukumu yao kwa masuala yote yasiyo ya Muungano katika mamlaka ya Washirika wa Muungano kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na Katiba za Washirika wa Muungano.
By Arnold Swai, Moshi

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger