Monday, January 21, 2013

SERIKALI YABADILI UTARATIBU WA MICHANGO SHULENI‏

Mheshimiwa Mwanri akipokea taarifa ya mradi wa maji ya kutega katika kijiji cha Kilida wilaya ya Mlele mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya miradi aliyoweka jiwe la msingi la ujenzi wa miradi hiyo,wilaya ya Mlele inakabiliwa na uhaba wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu ambapo wananchi wanaopata huduma ya maji ni asilimia ishirini na tano tu ya wakazi.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha KIlida wilaya ya Mlele mkoani Katavi wakiwa juu ya mti wakimsikiliza Mhe. Aggrey Mwanri, Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI alipokuwa katika ziara ya kikazi wilayani humo. Mhe Mwanri aliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji
ya kutega mlimani katika kijiji hicho.
Naibu Waziri TAMISEMI, Aggrey Mwanri akimuweka kitimoto Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda, Dr Kamgobe baada ya kulalamikiwa na akinamama kuwa wanatozwa pesa pindi wanapokwenda kujifungulia katika vituo vya huduma za afya vya serikali hasa zahanati katika mikutano ya hadhara wilayani humo, katikati mwenye suti ya bluu ni mkuu wa wilaya hiyo Paza Mwamlima.

Na Willy Sumia, Mpanda

SERIKALI imepiga marufuku tabia ya baadhi ya walimu kuwarudisha wanafunzi nyumbani kwa sababu ya kutolipia michango mbali mbali ya shule na kwa kukosa sare za masomo.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa, Mhe Aggrey Mwanri alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika uwanja wa Kashaulili mjini Mpanda akihitimisha ziara yake katika halmashauri ya mji wa Mpanda.

Alisema kumekuwa na mtindo kwa baadhi ya shule kuwarudisha wanafunzi nyumbani kwa kisingizio cha kukusanya michango lakini wanasahau kuwa muda ule ni muda wa masomo kwani siku na saa za masomo zimehesabiwa na inapopotea dakika moja kwa mwanafunzi kukaa bila kusoma haiwezi kufidiwa tena hivyo serikali imeliona na kuamua kuchukua hatua.

Alisema kuanzia jana (Januari 20,2013) hakuna kumrudisha mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari kwa sababu hajamalizia michango ya shule na wala eti kwa sababu hana sare za shule husika, badala yake walimu washirikiane na uongozi wa kata kuwawajibisha wazazi wasiokamilisha michango shuleni na kuwanunulia wanafunzi sare za masomo.

'' Walimu nisikilizeni, kuanzia leo hakuna ruhusa kwa mwalimu kumrudisha mwanafunzi nyumbani eti kutafuta michango, mnataka wakafanye vibarua huko? Mzigo wa michango ya shule na sare ni wa wazazi na walezi wao siyo wa mtoto tena msiwape barua watoto kuwapelekea wazazi wao, pelekeni katika ofisi za kata kuna kamati ya maendeleo ya Kata WDC" alisema Mhe. Mwanri

Alisema unapomrudisha mwanafunzi nyumbani akachukue mchango wa shule maana yake ni kwamba asirudi shule kama hajapewa mchango na hapo ndipo unadhoofisha maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma hivyo kama umeajiriwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huruhusiwi kuwarudisha wanafunzi wakatafute michango

Akizungumzia michango mingi mashuleni Mwanri alisema hivi sasa serikali imebadili utaratibu wa kurasimisha michango kwa kupitia ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa husika na hivyo kila shule itakayokaa na wazazi na kupanga michango yao ya shule kwa maendeleo ya shule yao lazima kwanza mapendekezo hayo yapelekwe kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo ili ayapitie mapendekezo hayo na kujiridhisha ndipo atoe kibali cha kuanza kutoza michango hiyo

Alisema hivi sasa kila shule ianze utaratibu wa kuita wazazi na kuangalia ichakavu wa madawati yaliyopo na kutolea mapendekezo ya ukarabati wake ili yaweze kutumika badala ya kuendelea na mtindo wa kila mwaka wanafunzi kudaiwa kwenda na madawati shuleni kwani kila mtu anajiuliza madawati hayo hayajai shuleni huko, ni bora uwepo utaratibu wa kuangalia mapungufu ndiyo yachangiwe na wazazi

Aliwaagiza wakurugenzi watendaji katika halmashauri kukagua na kujiridhisha namna majembe, mapanga na madawati yanavyotumika mashuleni kwani kuna baadhi ya sehemu wanafunzi wanaagizwa kwenda na majembe mapya yenye mpini lakini wakifika shuleni majembe mapya yanakusanywa na kuwekwa badala yake siku ya kulima ikifika wanafunzi wanagawiwa majembe ya zamani.

Naibu Waziri Mwanri anatarajia kukamilisha ziara yake katika mkoa wa Katavi Jumatano na kurejea mjini Dodoma kwa ajili ya kikao kijacho cha bunge.
MWISHO

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger