Saturday, February 9, 2013

Sh31 bilioni kujenga nyumba za walimu nchini


Kwa ufupi

Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha elimu ya Sekondari na Msingi nchini kote ikiwa ni pamoja na upungufu wa nyumba za walimu zinazohitajika.


KATIKA Mwaka wa Fedha wa 2012/13, Serikali imetenga kiasi cha Sh31 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu kupitia mpango wa bajeti za halmashauri, Bunge lilielezwa jana.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri ambaye alisema Serikali wakati wote itaendelea kukabiliana na changamoto za upungufu wa nyumba za walimu hadi itakapojiridhisha kuwa hali ni nzuri.

Naibu Waziri aliitaja changamoto kubwa inayoikabili Serikali kwa sasa ni ufinyu wa bajeti, jambo linalofanya ishindwe kutekeleza mambo mengi kwa muda unaokusudiwa.

Alikuwa akijibu swali la Ahmed Salum (Solwa-CCM), ambaye pamoja na mambo mengine alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la upungufu wa nyumba za walimu lililopo katika shule zote za Sekondari na Msingi katika jimbo la Solwa.

Katika swali la nyongeza, Richard Ndasa (Sumve-CCM) aliitaka Serikali ieleze mpango uliowekwa kuhusu fedha za rada kwenda mashuleni umefikiwa wapi na kwa nini Watanzania wasijulishwe.

Mwanri alisema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha elimu ya Sekondari na Msingi nchini kote ikiwa ni pamoja na upungufu wa nyumba za walimu zinazohitajika.

Alitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kupeleka fedha katika halmashauri, ambapo kati ya mwaka 2009/10 na 2012/13, Serikali imepeleka katika halmashauri zote Sh 13.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu na kati ya hizo Sh93 milioni zilipelekwa jimbo la Solwa.

Kuhusu fedha za rada, naibu huyo alisema mpango wake ulielekezwa katika ununuzi wa vitabu kwa shule,lakini sio katika majengo ambayo Ndasa alikuwa ameuliza, hivyo akasema si mahali pake katika kulijibu kwa wakati huu.    

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger