Na Anna Nkinda – Maelezo , Lindi
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete. |
Wazazi mkoani Lindi wametakiwa
kusimamia elimu ya watoto wao kwa kuhakikisha kuwa wanaenda shule, wanakagua
madaftari yao
na kuwarekebisha pale ambapo wamekosea kwa kufanya hivyo watafaulu vizuri
katika masomo na kufanikiwa kimaisha kwani elimu ni msingi wa maendeleo.
Wito huo umetolewa jana na mke wa
Rais Mama Salma Kikwete kwenye kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 36 ya
kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika kimkoa katika kata ya
Rondo wilaya ya Lindi vijijini.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mjumbe
wa Halmashauri kuu ya CCM taifa toka wilaya ya Lindi mjini alisema kuwa
maendeleo ya elimu si mazuri katika mkoa huo hivyo basi kina baba washirikiane
na wake zao kuhakikisha kuwa watoto wanahudhuria shule na kufanya vizuri katika
masomo yao.
“Ninyi watoto nawasihi msome kwa
bidii mkumbuke kuwa huu si wakati wa mtoto kukatisha masomo kwa ajili ya kupata
ujauzito kwani mkiwa na elimu kutakuwa na uhakika wa kupatikana kwa wataalamu
mbalimbali katika mkoa huu na kutatua tatizo la kutokuwa na wataalamu ambalo
limedumu kwa muda mrefu”, alisema Mama Kikwete.
Aidha Mjumbe huyo wa Halmashauri
kuu ya CCM taifa aliwataka wanawake kutosubiri nafasi za upendeleo za viti
maalum bali wagombee nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya chama ili
wafike katika ngazi ya maamuzi na kuachana na fikira kuwa wao hawawezi kumwaga
sera wakati wa uchaguzi.
Alimalizia kwa kuwataka wakazi wa
mkoa huo kudumisha amani, upendo na utulivu, kufanya kazi kwa bidiii, maarifa
na kujituma, wakulima walime kilimo cha kisasa ambacho kitawafanya wavune mazao
mengi zaidi pia wafanyakazi watumie muda wa kazi kufanya kazi na kuwahudumia
wananchi.
Mama Kikwete pia alifungua jengo
la ofisi ya CCM lenye thamani ya shilingi milioni 35 ambalo limejengwa na
Mbunge wa jimbo la Mtama ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa Benard Membe.
Waziri Membe alisema kuwa jengo hilo lina vyumba sita
ambavyo ni ofisi za jumuia zote za chama hicho ambazo ni Vijana, Wanawake,
Wazazi, pia kuna ofisi za Mbunge, Mjumbe wa NEC na chumba cha mikutano.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM
wa mkoa huo Ally Mtupa aliwataka wanachama wa chama hicho kuwa na mahusiano
mazuri baina yao
na viongozi wanaowaongoza. Wakisikia jambo wasiwe na papara ya kukimbilia
kuandamana bali wafanye upelelezi kwanza na wakishabaini ukweli ndipo wachukue
hatua.
Mtupa alisema, “Hivi sasa kuna
watu wanapita mitaani na kupotosha ukweli kuwa Serikali yetu haijaleta
maendeleo, wamesahau kuwa wanatembea katika barabara na kutibiwa katika
Hospitali zilizojenga na CCM, tunawaomba watu hawa wawaheshimu viongozi
wanaotawala kwani hata vitabu vya dini vinasisitiza umuhimu wa kuwatii viongozi
waliopewa mamlaka ya kutawala”.
Sherehe hizo zilienda sambamba na
mchango wa matembezi ya mshikamono ambapo zaidi ya shilingi milioni mbili
zilipatikana, ufunguzi wa ofisi za CCM, ufanyaji wa usafi wa mazingira , kuwatembelea
wagonjwa mahospitalini, utoaji wa kadi kwa wanachama wapya ambapo wanachama wa
kawaida 286 , jumuia ya wazazi 63 na kutoka vyama vya upinzani 23 walipewa kadi.
Asante sana MAMA SALMA KIKWETE kwa kazi nzuri unayoifanya ya kumsaidia kwa ukaribu na umakini MH.RAIS WETU na juhudi zako binafsi ambazo zinaanzia kwenye chama chetu pamoja na serikali yetu kwa ujumla
ReplyDelete