Wednesday, March 6, 2013

Pacha wa Kitanzania wenye vipaji vikubwa wang’ara Marekani



 
Vijana pacha wawili wa Kitanzania, Sylvanus na Salvanus wa umri wa miaka 21 wenye vipaji vya kipekee wanang’ara katika Chuo Kikuu cha Havard kilichoko Massachusetts, Marekani.

Salvanus anasomea udaktari wakati pacha wake, Sylvanus anasomea uhandisi kwenye chuo hicho.

Havard ni chuo kikuu cha bora cha tatu kwa ubora duniani, baada ya Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Massachusetts na kile cha Cambridge cha Uingereza.

Salvanus amekwishafanya upasuaji mkubwa kwa wagonjwa zaidi ya 14 huko Karatu na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Karatu, ambako pia upasuaji ulifanyika, Dk Lucas Kazingo alisema: “Hawa ni vijana wa ajabu, wana uwezo wa aina yake.”

Aliongeza: “Salvanus amefanya upasuaji katika hospitali hii, kwa mafanikio makubwa hapa na mwenzake huwa anamsindikiza. Kweli hawa ni vijana wa aina yake na ni hazina kubwa kwa taifa.”

Pacha hao ambao umahiri wao wa kutafiti umekuwa kivutio cha Kituo cha Utafiti wa Sayansi ya Anga cha Marekani (Nasa), wako likizo kwa sasa.

Salvanus yupo mwaka wa nne katika masomo yake ya udaktari. Sylvanus anasomea uhandisi wa kompyuta kwenye chuo hicho.

Vijana hawa wako nchini lakini chini ya uangalizi maalumu wa Serikali ya Tanzania na ile ya Marekani hasa kutokana na uwezo wao mkubwa wa kiakili.

“Vijana hawa, wamekuwa wakishirikiana katika kazi zao, ikiwamo ya udaktari na utafiti wa sayansi hali yao imewafanya sasa kuwa watu wa kipekee duniani,” alisema Dk Kazingo.

Salvanus yupo katika mazoezi ya udaktari kwa vitendo na kabla ya kutua nchini, pia alifanya majaribio hayo Botswana.

“Walikuja ofisini, nimezungumza nao, kweli ninachoweza kusema ni kwamba wana uwezo mkubwa na ndiyo maana wanasoma chuo cha watu wenye vipaji maalumu cha Havard,” alisema Dk Kazingo.

Wakizungumza na Mwananchi juzi, vijana hao ambao wamekuwa wakiishi pamoja kwa wakati mwingi, walisema walipata nafasi ya kwenda kusoma Marekani kutokana na msaada wa Rais Kikwete baada ya kupata taarifa za uwezo wao.

“Rais ndiye aliyetusaidia na anaendelea kutusaidia, hadi sasa tunaendelea vizuri na masomo,” alisema Salvanus.

Hata hivyo, vijana hawa hawakuwa tayari kuelezea historia na maisha yao kwa sasa... “Nadhani tutazungumza zaidi baada ya kuonana na Rais, kuna tafiti tumefanya ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa.” Aliongeza Salvanus.

Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Adam Akyoo alisema kwa sasa mamlaka hiyo, ndiyo imepewa jukumu la kuwasimamia vijana hao hadi watakaporejea chuoni.

Kutokana na hali hiyo wanatumia jina la Kawasange, pengine kama njia ya kuficha jina lao la ukoo wao kwa sababu za kiusalama.

Jina hilo ni la Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Ngorogoro anayeitwa Bruno Kawasange, ambaye ndiye mwangalizi mkuu wa vijana hao.

Akyoo alisema kabla ya kwenda Havard, walikuwa wakisoma Shule ya Sekondari Ilboru, Arusha mwaka 2004 hadi 2005. Pia walisoma Shule ya Msingi ya Arash wilayani Ngorongoro mwaka 1997 hadi 2003.

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger