Rais Jakaya Kikwete akiangalia shughuli za uzalishaji umeme hivi karibuni, mkoani Mtwara |
KWA UFUPI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alisema jana kuwa ujenzi huo unaofanywa na Kampuni ya China Petroleum and Technology Development Co-operation (CPTDC), ambao awali, ulipaswa kuanza wiki iliyopita, umeanza juzi baada ya Serikali kufikia mwafaka na wananchi wa Kijiji cha Msimbati kinapojengwa.
HATIMAYE ujenzi wa kiwanda cha kusafisha gesi kabla ya kusafirishwa
kwenda Dar es Salaam umeanza mkoani Mtwara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi
alisema jana kuwa ujenzi huo unaofanywa na Kampuni ya China Petroleum and
Technology Development Co-operation (CPTDC), ambao awali, ulipaswa kuanza wiki
iliyopita, umeanza juzi baada ya Serikali kufikia mwafaka na wananchi wa Kijiji
cha Msimbati kinapojengwa.
“Mkuu wa Wilaya ya Mtwara (Wilman Ndile) na vijana wake
walilazimika kufika Kijiji cha Msimbati, ambako wananchi walikuwa na mgogoro na
watu wa Marine Park,” alisema Maswi.
Alisema baada ya ziara hiyo kushindwa kufanyika Jumapili
iliyopita, uongozi wa wilaya ulikutana na viongozi wa kijiji na kufikia mwafaka
uliofanikisha kuanza kwa ujenzi huo.
Alisema kuanzia mradi huo kutatoa ajira za kawaida kwa
wakazi saba wa maeneo yanayozunguka mradi huo na kwamba kazi hiyo itaongeza
mahitaji ya bidhaa mbalimbali na huduma katika Kata ya Msimbati
“Mathalan kuku, matunda na mboga za majani vinahitajika
sana. Sasa wananchi ambao awali, hawakutaka kuelezwa lolote, wameanza
kuchangamkia fursa hizo jambo ambalo litawanufaisha zaidi,” alisema.
Ujenzi huo ulielezwa kuwa unatekelezwa sambamba na mwekezaji
kujenga visima vitatu vya maji safi na salama kijijini Madimba.
Alisema mwekezaji pia atasambaza umeme kwa kaya 300 za ndani
na jirani ya kijiji hicho na kwamba vifaa vitakavyotumika katika kazi hiyo
vinatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu.
Maswi alisema shule zote kwenye Kata ya Msimbati kikiwamo
Kijiji cha Madimba, zitakarabatiwa na mwekezaji huyo ikiwa ni sehemu ya mpango
wa wananchi waishio maeneo ya mradi kunufaika na uwekezaji.
Hata hivyo, habari nyingine zinaeleza kuwa ulinzi
umeimarishwa katika eneo hilo la mradi ili kuhakikisha hali ya usalama
inaendelea kuwapo.
Mgawo wa umeme
Akizungumzia kuhusu kukatika mara kwa mara kwa umeme katika
maeneo mengi nchini hali inayowafanya wananchi kuamini kuwa kuna mgawo wa umeme
kinyemela, Maswi alisema kamwe Taifa halitaingia gizani.
Alisema kukatika kunakotokea sasa kumesababishwa na kazi za
kiufundi zilizotarajiwa kukamilika jana jioni... “Kwa taarifa nilizonazo,
mtambo mdogo uliopo Ubungo unabadilishwa na kuwekwa mkubwa, pia Kipawa kuna
matengenezo ya transfoma ili kuwezesha usambazaji wa umeme hadi Kisarawe na
nyie mnaweza kwenda mkashuhudia kinachoendelea.”
Hata hivyo, taarifa kutoka Mikoa ya Kilimanjaro, Dodoma,
Morogoro, Arusha na Mwanza zinasema kumekuwa na tatizo kubwa la umeme kwa wiki
mbili sasa.
No comments:
Post a Comment