Sunday, April 7, 2013

Tume iliyoundwa na Katibu Mkuu wa CCM yatua Loliondo



KWA UFUPI

Wiki moja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki kugonga meza na kusema Serikali haitabadili msimamo wake kuhusu kuchukua ekari 1,500 za eneo la pori tengefu la Loliondo, timu ya viongozi wa CCM ya kuchunguza mgogoro huo imesema uamuzi huo wa Serikali unakiuka sheria na una athari kwa wananchi wa Loliondo.

Loliondo na Dar. 
Wiki moja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki kugonga meza na kusema Serikali haitabadili msimamo wake kuhusu kuchukua ekari 1,500 za eneo la pori tengefu la Loliondo, timu ya viongozi wa CCM ya kuchunguza mgogoro huo imesema uamuzi huo wa Serikali unakiuka sheria na una athari kwa wananchi wa Loliondo.

Kamati hiyo inayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, imeamua kuupeleka mgogoro huo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda baada ya kujiridhisha kuwa uamuzi wa Serikali kutwaa ardhi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,500 unakiuka sheria.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari wa Machi 26, 2013 Waziri Kagasheki alisema ili kutatua migogoro iliyopo, kunusuru ikolojia ya Hifadhi za Serengeti, Ngorongoro na pori Tengefu Loliondo, Serikali imeamua kutoa kilometa za mraba 2,500 kwa wananchi kuwa vijiji na wa kilometa za mraba 1,500 zitabaki serikalini.

Waziri Kagasheki alisema kufanya hivyo kutasaidia kulipa hadhi pori tengefu kwa ajili ya kulinda mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi na taifa.

Timu ya CCM

Wajumbe wa tume hiyo, iliyoundwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana pia yumo Chiristopha Ole Sendeka (Mbunge-Simanjiro), Lekule Laizer (Longido) na Mary Chatanda ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha.

Akizungumza na wananchi wa Loliondo katika Kijiji cha Olorien Magaiduru, Nchemba alisema baada ya kupokea maelezo kutoka kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo, viongozi wa mila na Serikali wa ngazi mbalimbali wamejiridhisha kuwa hoja za wananchi kupinga uamuzi wa Serikali zina nguvu.

“Tumeambiwa bila eneo hili kubaki kwa wananchi hakuna maisha, kwani eneo hili ndiyo tegemeo kwa maji na malisho ya mifugo yenu, katika hili nakubaliana nanyi kwani ardhi ndiyo uhai wenu,” alisema Nchemba.

Alisema kutokana na CCM kujikita katika kutetea masilahi ya wananchi kwa kuamini kuwa masilahi ya wananchi ndiyo ya chama hicho, japo kuwa waziri ndiye aliyetangaza uamuzi wa Serikali, lakini CCM inatazama uzito wa jambo lenyewe.

“Mwenye duka anapomwachia mtu duka na yeye akapandisha bei na hivyo kufanya wateja kuanza kuhama ni lazima mwenye duka arudi, ili duka lisifungwe hivyo hatutakubali tukose wateja, lazima tumdhibiti muuza duka,” alisema Nchemba na kueleza mwenye duka sasa ni CCM.

Alisema baada ya kupokea maoni ya wananchi, watapeleka taarifa ya timu yao kwa Kinana na baadaye kwa Waziri Mkuu na kama ikishindikana kutolea ufafanuzi watapeleka taarifa yao kwa Rais Jakaya Kikwete.
Naye Christopha ole Sendeka alisema, uamuzi wa Waziri Kagasheki kulitangaza eneo la vijiji vya Tarafa ya Loliondo na Sale kuwa ni pori tengefu ni ukiukwaji wa sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 ambayo ilipitishwa na Bunge.

Alisema haiwezekani waziri kutangaza eneo hilo kuwa pori tengefu wakati kuna vijiji vyenye hati miliki katika eneo hilo hilo na havijashirikishwa.

“Hatukuja hapa kupiga siasa kwani huwezi kupiga siasa mbele ya jeneza la watu zaidi 65,000,” alisema Sendeka.

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger