Friday, May 24, 2013

CCM yataka walioshindwa kuendesha viwanda wanyang’anywe


KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeagiza Serikali kufanya tathimini ya viwanda vilivyobinafsishwa na kuvitambua vilivyofungwa ili kuandaa utaratibu wa kuwapa watu wenye uwezo kuviendesha.

Akiozungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana Katibu Mkuu wa NEC- Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro alisema Kamati Kuu iliyokutana juzi mjini hapa nchini ya Rais Jakaya Kikwete pamoja na mambo mengine ilitafakari masuala yanayohusu uchumi.

Dk Migiro alisema kuuzwa kwa mashirika na viwanda vya umma kwa watu na makampuni binafsi kumekuwa na matokeo ya aina mbili, kuna yale yaliyobinafsishwa na kuwa na maendeleo mazuri na kuchangia uchumi wa Taifa na yake ambayo yanaendeshwa kwa kiwango cha chini au yamefungwa.

“Kamati kuu inasikitishwa na hali hii kwani viwanda vilivyofungwa ni vile vilikuwa vikifanya kazi muhimu ya uzalishaji kama korosho, usindikaji wa pamba, mafuta ya kula, viwanda vya mazao ya ngozi na vinginevyo, hali hii inalikosesha taifa fursa za ajira kwa mapato, kuimarika kwa uzalishaji na kuongezeka kwa uuzaji wa bidhaa zilizosindikwa na kuuzwa nchini,” alisema.

Alisema imedhihirika wafanyabiashara waliochukua viwanda hivyo ndiyo wanaofanya biashara ya kununua mazao ya kilimo na mifugo na kuuza nje kama bidhaa ghafi wakati huo huo wakiwa wamevifunga viwanda hivyo.

Alisema kutokana na hali hiyo kamati kuu inaiagiza Serikali kufanya tathimini ya viwanda vilivyobinafsishwa ili kuvitambua, vile vilivyofungwa na kuwataka waliouziwa wavifungue na iwapo watashindwa kutimiza masharti yaliyowekwa, Serikali iandae utaratibu wa kuwapa wenye uwezo wa kuviendesha.

Akizungumzia migogoro ya Kidini alisema kamati Kuu inaipongeza Serikali na vyombo vya dola kwa namna inavyoendelea kukabiliana na wahalifu wanaotumia mgongo wa dini kuanzisha vurugu na uvunjifu wa amani nchini na kuwataka Tanzania kukataa vitendo vyote vinavyochochea migogoro ya kidini na wananchi kujihadhari na watu wenye nia ya kuligawa taifa.

Dk Migiro alisema kuwa pamoja na jitihada zilizofanyika Kamati Kuu inaitaka Serikali kuandaa mikakati ya kuzuia migogoro ya kidini kabla haijajitokeza.

Juu ya suala la migogoro ya wakulima na wafugaji alisema migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa mingi na kuenea sana nchini na imekuwa ikitokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la idadi ya watu na mifugo.

Alisema kutokana na hali hiyo, Kamati kuu imeiagiza Serikali kushughulikia na kuitafutia ufumbuzi wa kudumu migogoro hiyo na kuharakisha zoezi la kutenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji, kujenga majosho ili kuwezesha wafugaji kutohamahama na mifugo yao.

Pia alibainisha, Kamati kuu imeiagiza Serikali kushughulikia mgogoro wa wakulima wadogo wa miwa na kuupatia ufumbuzi wa kudumu matatizo ya wakulima hao haraka iwezekanavyo pia Serikali kutafuta utaratibu bora zaidi na wenye tija wa kuwafikishia wakulima mbolea kwa wakati na kwa uhakika.

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger