Tuesday, June 25, 2013

Kauli ya Polisi kubana wakaidi yasisitizwa

Stephen Wasira
Stephen Wasira

 


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Uratibu na Mahusiano, Stephen Wasira, ameunga mkono kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ya kutaka wanasiasa na wafuasi wao watakaokaidi amri halali, kuchukuliwa hatua. 


Akizungumza jana wakati akichangia Bajeti ya Serikali, Wasira alisema amani ina uhusiano na maendeleo na haina vyama vya siasa, bali ni ya Watanzania. “Tuache ushabiki wa vyama, amani haina vyama ni ya Watanzania wote, kama mnadhani ina vyama, basi nendeni katika uchaguzi muombe kura ili mvuruge amani kama mtaipata,” alisema. 

Alikumbushia swali la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF), katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu, alipohoji kwa nini Pinda aliruhusu raia wapigwe, wanapokaidi amri halali, wakati Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inakataza Serikali kupiga raia na kumdhalilisha. 

Pinda katika jibu lake, alisema kuna tofauti ya mtuhumiwa aliyefikishwa katika vyombo vya sheria, ambaye Katiba inakataza kufanywa chochote, lakini anayekaidi amri halali lazima ashurutishwe kuitii. “Lazima uweke tofauti ya aliyekamatwa na aliyefikishwa katika vyombo vya sheria, ambaye Katiba inasema asifanywe chochote, lakini ukiambiwa usiandamane, ukaamua kuandamana na sisi tutakwenda hivyo hivyo mpaka tujifunze kutii sheria bila shuruti,” alionya. Akiongeza majibu yake katika swali hilo, Wasira alihoji ni kifungu gani cha Katiba kinachoruhusu ukaidi. “ Bunge linatunga sheria na ukaidi ni kuvunja sheria, inakuaje sheria mlizotunga wenyewe, mtu akivunja akachukuliwa hatua mnalalamika?

 “Huwezi kusoma aya moja katika Korani na kujenga Msikiti wako, wala kuanzisha Kanisa lako kwa kutumia mstari mmoja wa Bibilia,” alisema na kutaka wanasiasa, kuacha kujificha katika kivuli cha Haki za Binadamu, wakitaka haki zao zisivunjwe, lakini wao wakivunja za wenzao. “Mimi nauza nyanya na wewe unaandamana unakanyaga nyanya zangu, nikikuuliza unasema unatekeleza matakwa ya demokrasia, demokrasia gani hiyo ya kukanyaga nyanya zangu?” 

Alihoji. Alikumbushia kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwamba demokrasia bila nidhamu ni ghasia na kuongeza kuwa mfumo wa vyama vingi, ni wa hoja si vurugu. “Kama una hoja kuhusu elimu nenda kaseme kuwa tulisema tutatoa elimu, lakini si bora, sisi tutasema tulianza na shule sasa tunapandisha ubora, wewe twambie kama utafuta shule za kata kwanza na hiyo ndiyo demokrasia. “Fujo haiwezi kuwa hoja, sema hoja toa hoja, wakubwa waliotufundisha demokrasia Marekani, wao wanatoa hoja tena bungeni… utasikia Waziri Mkuu ulituahidi kile na kile, lakini hakipo, na yeye anajibu tumeanza na hiki, hiki na tunakusudia kwenda kule,” alisema Wasira. 

Wizi kwa mujibu wa sheria Waziri huyo pia alikosoa Sheria ya Manunuzi na kusema inatumiwa vibaya na watendaji hasa katika Bodi za Zabuni, kuiibia nchi kwa mujibu wa sheria. 

Alihoji kwa nini bidhaa na huduma zinazonunuliwa na Serikali kupitia sheria hiyo ziwe ghali, kuliko zinazonunuliwa na sekta binafsi. “Kwa nini maji yanayonunuliwa kwa zabuni, yawe ghali kuliko ninayonunua mtaani, hii Sheria ya Manunuzi inanunua wapi na mimi nanunua wapi?” Aliendelea kuhoji. 

Alisema Bajeti ya Serikali ya Sh trilioni 18 na sehemu ya maendeleo ya Sh trilioni 5, asilimia 70 inakwenda katika ununuzi, lakini sheria hiyo inakwamisha maendeleo kwa kusababisha Serikali iuziwe bidhaa na huduma kwa bei ghali na kupendekeza sheria hiyo irudishwe bungeni ifanyiwe marekebisho ya haraka.

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger