Friday, July 12, 2013

Kikwete afungua kongamano la kutafuta amani lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

JK ahadharisha wanahabari

Akitoa mfano, Kikwete alisema nchi za Rwanda na Kenya ni mifano hai kwa kuwa kuna waandishi wa habari ambao walishtakiwa pamoja na wanasiasa kwa uchochezi na kusababisha machafuko. image

Dar es Salaam.


Rais Jakaya Kikwete ametoa wito kwa waandishi wa habari kutoandika habari zenye kuchochea vurugu kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kujikuta wakiwa matatani.
Kikwete alisema hayo juzi wakati akifunga kongamano la kutafuta amani lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
“ Unaweza kuandika au kutangaza habari ya uchochezi leo, lakini vurugu zikitokea hata kama ni baada ya miaka 20 utatafutwa na kushtakiwa kwa habari hiyo,” alisema Kikwete. Akitoa mfano, Kikwete alisema nchi za Rwanda na Kenya ni mifano hai kwa kuwa kuna waandishi wa habari ambao walishtakiwa pamoja na wanasiasa kwa uchochezi na kusababisha machafuko.
“Nawakumbusha waandishi kuweni makini kwa habari mnazoziandika na kuzitangaza kwa kuwa mna uwezo wa kujenga na kubomoa,” alisema.
Alisema vyombo vya habari,siasa na dini vikitumiwa vibaya ni rahisi kusababisha vurugu zenye kuhatarisha maisha ya wananchi.
Alitaka TCD kuandaa kongamano kama hilo kwa ajili ya waandishi wa habari wakiwa ni wadau katika kutafuta amani.
Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia akitoa maazimio ya kongamano hilo, alisema viongozi waandamizi wa serikali wajizuie kutumia lugha za vitisho.
Alisema pia kongamano hilo limeazimia kwamba kituo hicho kiwe karibu na vyombo vya habari na kuwahimiza kuandika habari zenye uzalendo na mshikamano wa kitaifa.

Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger