Friday, July 26, 2013

Maabara ya kisasa Bagamoyo : Kifaa tiba muhimu kwa Tanzania, Afrika.

Kukamilika kwa maabara hiyo nchini kutachochea ugunduzi na kujenga jukwaa la ushirikiano wa pamoja katika kukabiliana na maradhi ya kuambukiza na kutengeneza mtandao wa taarifa zitakazosaidia kuhuisha udhibiti wa maradhi mbalimbali kwa manufaa ya jamii”.



Maabara ni sehemu muhimu kwa tiba yoyote ile Bagamoyo

- Kitabibu inaitwa maabara daraja la tatu au kwa kitalaam ‘Bio-safety Level 3 (BSL3)’ ni moja kati ya maabara ya kisasa kabisa zaidi katika uchunguzi wa bakteria na virusi wa aina mbalimbali ambayo Tanzania imepata bahati ya kuwa nayo baada ya uzinduzi wa hivi karibuni.

Maabara hiyo imepatikana kwa ushirikiano baina ya serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wahisani wa Shirika la Wahisani wa Maendeleo la Italia, Taasisi ya Kupambana na Maradhi ya Kuambukiza ya Italia (INM) ‘Spallanzani’ na taasisi ya Italian National Institute for Infectious Diseases INMI “Spallanzani”. 

 Serikali na wahisani hao pamoja na Kituo cha Utafiti cha Ifakara (IHI) wamefanikisha kuwepo kwa maabara hiyo ambayo imegharimu zaidi ya Sh1.2 bilioni na kulingana na tafiti mbalimbali maabara kama hiyo ni ya tatu kwa Afrika

Nchi zingine ambazo zinatajwa kuwa na maabara kama hiyo ni pamoja Nigeria iliyozindulia 2010 na Afrikas Kusini iliyozinduliwa 2011. Kulingana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid kuwepo kwa maabara hiyo nchini kunafungua ukurasa mpya katika sekta ya afya kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Dk Rashid anasema wakati wote serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kusafirisha sampuli za kibaiolojia nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara ili kubaini aina ya ugonjwa usiofahamika ambao unakuwa umeibuka katika eneo fulani fulani sasa hali itakuwa tofauti.

“Ni kifaa tiba muhimu ambacho nchi imepata katika historia ya tiba nchini na tunaamini kuwa itasaidia udadisi, utafiti, uchunguzi na hatimaye ugunduzi wa maradhi mbalimbali kabla ya kujua tiba stahiki” anasema.


Anabainisha kuwa licha ya uchunguzi wa maradhi hayo lakini pia itakuwa ni darasa zuri na muhimu kwa wanafunzi wa afya na watafiti wengine katika kubaini na kutambua lakini pia kuweza kufanya ugunduzio wa tiba mpya za maradhi mbalimbali.

Meneja wa Mpango wa maabara hiyo, Francesco Vairo anasema maabara hiyo itakuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kubaini virusi na bakteria wa maradhi mbalimbali ikiwa ni pamoja na magonjwa mapya na ya milipuko kama vile Ebola, virusi vya Sars, Dengeu, Homa ya Bonde la Ufa na maradhi mengine.

 Anasema pia maabara hiyo kwa kushirikiana na IHI wanafanya utafiti wa chanzo ya Malaria na Ukimwi na kukamilika kwake anasema kitakuwa kichocheo muhimu katika utafiti wa kimaabara hususani katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara kutokana na msongamano unaotokana na ukuaji wa miji yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya milipuko ya magonjwa ya zamani na mapya ambayo utambuzi wake unahitaji maabara za kisasa” anasema.

Anaongeza kuwa maabara hiyo ipo katika viwango ambavyo vinamhakikishia mtu wa maabara anakuwa salama wakati wote wa utafiti, sampuli zinazofanyiwa uchunguzi zinaharibiwa baada ya kutumika na uhifadhi wa kumbukumbu na takwimu zingine kwa ajili ya matumizi ya baadae.

Vairo anabainisha kuwa maabara hiyo ina viwango vyote vya kuhakikisha usalama kwa wafanyakazi wa maabara, watu wanaofanya shughuli zao jirani na maabara hiyo na hata mazingira yanayozunguka maabara lengo likiwa ni kudhibiti maambukizi. 

 “Hakuna sampuli ambayo inaweza kusababisha maambukizi ambayo itatoka nje ya maabara na kuleta athari kwa wanajamii,” anasema na kuongeza kuwa kuna mfumo ambao unaharibu na kuondoa kabisa uwezekano huo anasema na kuongeza kuwa ni wazi kutakuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya afya nchini.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), , Rufaco Chatora anasema dunia siku za karibuni imeshuhudia kuibuka kwa maradhi mengi mapya ambayo ili kuyatambua na kujua hatua za kuchukua ni lazima kuwa na maabara za kisasa.

Anatoa mfano wa kubainika kwa virusi vinavyofanana na vile vya ugonjwa wa Sars vilivyobainika nchini Saudi Arabia hivi karibuni kuwa ni moja ya changamoto ambazo zinahitaji maabara na vifaa vya kisasa ili kuepusha vifo na kuwahakikishia wakazi afya njema.

“Kuwepo kwa maabara kama hii mkunasaidia kuifanya Tanzania kama Taifa kuweza kupiga hatua kuelekea malengo ya milenia 2015 upande wa afya” anasema Chatora na kuongeza kuwa utafiti wa kimaabara ni muhimu katika kukabiliana na maradhi ya hatari ya milipuko.

Katibu wa Afya Wilaya ya Bagamoyo, Bonaventure Sagamila anasema maabara hiyo ni ufunguo mwingine wa kuitambulisha wilaya hiyo ulimwenguni katika sekta ya afya kwani anaamini kuwa itapokea wageni wengi ambao watakuja katika utafiti na ugunduzi mpya ni jambo linalotarajiwa.

“Ni hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya afya na ninaamini kuwa ugunduzi wa tiba na maradhi mapya ambayo awali hayakufahamika ni vitu ambavyo vinaweza kutokea Bagamoyo sasa,” anasema Sagamila.
Na Joseph Zablon, Mwananchi

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger