Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete
akimkabidhi bajaji mpya mlemavu wa miguu ambaye ni mfanyakazi wa TANROADS
Bi.Sarah Nalingigwa Nkumbo huko ikulu mjini Dodoma leo asubuhi. Kulia ni Waziri wa Ujenzi
John Pombe Magufuli.Wapili kushoto ni mke wa Rais Mama Salma Kikwete na kushoto
ni mkurugenzi Mkuu wa TANROADS Injinia Patrick Mfugale. Bi. Sarah ambaye ni
Mfanyakazi wa TANROADS mkoani Singida alikabidhiwa Bajaji hiyo ikiwa ni ahadi
ya Rais alipokuwa akifungua Barabara ya Manyoni- Itigi.(picha na Freddy Maro)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumapili, Februari 10, 2013
amekabidhi pikipiki aina ya bajaj kwa mama mmoja mlemavu, Mama Sarah Mkumbo
Nalingigwa katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu Ndogo mjini Dodoma.
Mama Nalingigwa ni mtumishi wa
Wakala wa Barabara nchini – TANROADS- katika Mkoa wa Singida na shughuli ya leo
imehudhuriwa pia na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Mtendaji
Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mufugale na Mama Salma Kikwete.
Shughuli ya makabidhiano ya leo,
inatimiza ahadi ambayo Mheshimiwa Rais aliitoa kwa Mama Nalingigwa wakati
alipokutana naye miongoni mwa wananchi waliohudhuria sherehe ya utiaji jiwe la
msingi kwenye ujenzi wa Barabara ya Manyoni-Itigi=Chaya mjini Itigi, Mkoa wa
Singida Novemba mwaka jana.
Akizungumza mara baada ya
kukabidhi pikipiki hiyo, Rais Kikwete amemwambia mama huyo: “Nimefurahi kwamba
nimeweza kutimiza ahadi yangu. Hii ndiyo faraja yangu kwamba sasa utaweza
kufanya kazi zako kwa urahisi zaidi, utaweza kutembea kwa urahisi zaidi na
kufika kazini na kurejea nyumbani kwa namna ya haraka zaidi.”
Naye Mama Nalingigwa amewwambia
Rais Kikwete: “Wewe ni kiongozi shupavu, kiongozi hodari na mpiganaji
anayemjali kila mtu. Nakuombea kwa Mwenyezi Mungu akujalia ili uendelee kuwaona
wengine wenye mahitaji kama ya kwangu.”
Ameongeza mama huyo ambaye amefanya
kazi Wizara ya Ujenzi kwa miaka 30 iliyopita: “Kwa kuniwezesha kiasi hiki,
umenipa uwezo wa kufanya kazi kwa namna bora zaidi., Ni vyema kuwa viongozi
wengine wakaiga mfano wako wa kujali watu walioko chini yako.”
Amesisitiza: “ Sisi walemavu tuna
mahitaji mengi na hivyo naomba unedelea kutuangalia kwa jicho la huruma na
kutupunguzia vikwazo vya maisha kila nafasi inapojitokeza.”
No comments:
Post a Comment