Sunday, May 5, 2013

DEREVA WA “BODA BODA” AKAMATWA NA SHORTGUN, RISASI SITA



Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Jeshi la Polisi Mkoani hapa limemkamata mtu mmoja aitwaye Ally Rashid Salimu (23) Mwendesha pikipiki za abiria maarufu kwa jina la “Boda Boda” mkazi wa kata ya Sombetini jijini hapa akiwa na bunduki aina ya shortgun Mossberg yenye namba T292166 ikiwa na risasi sita.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake 30/04/2013 saa 5:30 asubuhi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas alisema kwamba, tukio hilo lilitokea juzi tarehe 28.04.2013 muda wa saa 3:00 asubuhi katika maeneo ya Shamsi yaliyopo jijini hapa.

Alisema siku ya tukio dereva huyo wa pikipiki akiwa katika eneo hilo alikuwa anaendesha pikipiki aina ya Skymark yenye namba za usajili T. 615 BZL huku akiwa amebeba begi lilionekana kutuna sana, ndipo askari waliokuwa doria katika eneo hilo walimtilia shaka na kisha kumfuatilia na kufanikiwa kumsimamisha.

“Mara baada ya kumsimamisha askari hao walipekua begi hilo na kukuta silaha hiyo ikiwa na risasi sita na kisha kumfikisha mtuhumiwa huyo katika kituo kikuu cha polisi cha hapa Arusha mjini”. Alifafanua Kamanda Sabas.
Kamanda Sabas alisema upelelezi juu ya tukio hilo bado unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani pindi utakapokamilika.

Tukio hilo la ukamataji wa bunduki hiyo limekuja wiki tatu tu baada ya jeshi hilo kukamata bastola moja pamoja na risasi 41 kutoka kwa watuhumiwa waliokuwa wanahusishwa na matukio ya kumjeruhi Sister Mary Shobana na kisha kumnyang’anya fedha taslimu Tsh 30,000,000/= (Milioni thelathini) eneo la Notre Dame Njiro lililopo jijini hapa, fedha ambazo alitoka kuchukua benki ya Exim tawi la Shoprite.

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger