Sunday, May 26, 2013

Nyerere, Kawawa kutambuliwa AU

Mwalimu Julius Nyerere,Mama Maria Nyerere na familia yao.


Mzee Rashidi Kawawa
BABA wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ni miongoni mwa Watanzania watatu wanaotarajiwa kutambuliwa na kuenziwa na Umoja wa Afrika (AU) rasmi kama Mwafrika Mashuhuri wa Kimajumuia.
Hatua hiyo inatokana na kuheshimu mchango wao katika mapambano ya Uhuru wa Afrika na kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao sasa unajulikana kama AU.

Watanzania wengine katika kundi hilo la ‘Mwafrika Mashuhuri’ ni Rashidi Kawawa na Sebastian Chale, Katibu Mkuu wa Kwanza wa Sekretarieti ya Kamati ya Ukombozi wa OAU, ambao kwa sasa ni marehemu.

Kutokana na mchango wa Nyerere katika Umoja huo, mjane Mama Maria Nyerere amealikwa kuhudhuria sherehe za miaka 50 ya Umoja huo uliozaliwa Juni 25, 1963, akiwa katika kundi la wageni maalumu wa kimataifa na kikanda wa Bara la Afrika.

Wengine walioalikwa na kuwasili juzi wakiwa sehemu ya ujumbe wa Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya sherehe hizo ni marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, wakiwa miongoni mwa marais wote wastaafu wa Afrika walioalikwa.

Ujumbe wa Tanzania katika sherehe hizo unawashirikisha pia Dk Salim Ahmed Salim, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja huo kwa muda mrefu zaidi wa miaka 12 kuliko Katibu Mkuu mwingine, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha-Rose Migiro na aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya OAU kusini mwa Afrika, Brigedia Jenerali Hashim Mbita.

Wakati wa uongozi wa Dk Salim, ndipo OAU ilipofanyiwa marekebisho na mabadiliko makubwa, kutoka OAU na kuwa AU.

Aidha, AU imealika watu mashuhuri walioliletea Bara la Afrika heshima na sifa kupitia siasa, michezo, muziki na uongozi wa jumuiya za Umoja huo, wakiwamo Watanzania, Getrude Mongela ambaye alikuwa Spika wa Kwanza wa Bunge la Afrika, Dk Rosebud Kurwijila ambaye ni Kamishna Msaidizi wa Masuala ya Kilimo na Uchumi wa Kamisheni ya AU, na Jenerali Ulimwengu ambaye alikuwa kwa miaka mingi akiiwakilisha Tanzania katika Umoja wa Vijana wa Afrika mjini Algiers, Algeria.

Kwa mujibu wa ratiba ya ziara ya Rais Kikwete, jana alitarajiwa kushiriki Mkutano Maalumu wa Wakuu wa Nchi za AU na sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya kuzaliwa kwa Umoja huo na leo atahudhuria Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU ambao umepangwa kuendelea kwa siku mbili.

By Mwandishi Maalumu, Addis Ababa   

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger