Wednesday, May 22, 2013

TAARIFA KUHUSU MATANGAZO YA KAZI SERIKALINI


 


Waombaji waliotuma maombi ya fursa za ajira kwa ajili ya matangazo yaliyokuwa yametolewa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma  kwa niaba ya Waajiri mbalimbali nchini mnamo  tarehe 26 Machi, 2013 moja likiwa katika lugha ya Kiingereza na lingine katika lugha ya Kiswahili ambapo mwisho wa kutuma maombi ilikuwa tarehe 9 Aprili, 2013 wametakiwa kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira mara kwa mara ili kupata ratiba ya usaili kwa nafasi walizoomba.


Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Bw. Xavier Daudi amesema  hayo leo alipokuwa akiongea na baadhi ya wadau waliomtembelea ofisini kwake wakitaka ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu mchakato wa Ajira Serikalini.

Amesema ofisi yake itaendelea kuwafahamisha wale wote walioomba  nafasi za kazi Serikalini kadri siku zinavyosogea. Amebainisha kuwa kwa tangazo la kiingereza lililotolewa tarehe 26 Machi, 2013 ambalo lilihusu Taasisi za Umma  zaidi, usaili wake utaanza tarehe 20 mwezi huu kama ratiba ilivyoainisha katika tangazo la kuwaita kwenye usaili lililotolewa tahere 16 Mei, 2013 kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Ajira likibainisha usaili utafanyika tarehe ngapi na sehemu gani pamoja na orodha ya majina ya wahusika waliokidhi vigezo vya tangazo kwa  nafasi hizo.

 Daudi  amewataka waombaji wa tangazo lililokuwa limetolewa kwa lugha ya Kiswahili tarehe tarehe 26 Machi, 2013 waendelee  kuvuta subira kwani ratiba yake ya Usaili kwa waombaji wenye Sifa itatolewa mara baada ya Usaili wa Tangazo la Kingereza kukamilika ili kuepuka kuwachanganya waombaji. Pamoja na hayo amewataka waombaji hao kukaa tayari kwani usaili wa tangazo hilo unaweza kufanyika wakati wowote mwezi Juni mwaka huu ila tarehe rasmi na wapi watajulishwa baadae.

Aidha, Waombaji wa nafasi wazi za kazi  kwa tangazo la kazi lililotolewa kupitia tovuti hii tarehe  16 Aprili, 2013 ambalo mwisho wake wa kutuma maombi ilikuwa tarehe 2 Mei, 2013,  wanafahamishwa kuwa mchakato wa kuchambua maombi yao bado unaendelea na watapewa taarifa ya kuitwa kwenye usaili kwa wale waliokidhi vigezo vya tangazo mara baada ya taratibu zote kukamilika.

Katibu huyo pia ametoa Rai kwa waombaji wote waliochaguliwa kuja kufanya usaili kujiandaa vyema ikiwa ni pamoja na kuzingatia vitu muhimu wanavyopaswa kuja navyo kwenye usaili ikiwemo vyeti vya Kitaaluma.

Daudi alimalizia kwa  kuwatahadharisha waombaji wa fursa za Ajira serikalini pamoja na wadau  kuwa makini na baadhi ya Matangazo ya Ajira ambayo yanatolewa kupitia   baadhi ya mitandao ya kijamii hususani wa  www.eastafricajobscareer.com yenye lengo la kupotosha jamii. Ofisi yake imefikia hatua ya kusema haya kutokana na mtandao huo alioutaja hapo juu kuchukua matangazo ya taasisi yake na kuyabadilisha tarehe za kutolewa, mwisho wa kutuma maombi, kumbukumbu namba pamoja na vichwa vya habari na kuyaweka hewani ilihali wakijua wazi hayajatolewa na Sekretarieti ya Ajira.

Hivyo amewataka wadau wote kuyapuuza matangazo hayo ya uongo yenye nia ya kuwapotosha. Aidha, amewahimiza wananchi pindi wanapoona matangazo ya kazi yanayoihusisha Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma katika mitandao au mbao za matangazo kujiridhisha ili kuyathibitisha kupitia  tovuti ya www.ajira.go.tz ili kuwa na uhakika zaidi kuliko kudanganywa na kutuma barua za maombi kwa matangazo ambayo si ya kweli.


Imetolewa na  Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Ofisi ya Rais-Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma
Kwa maelezo zaidi; wasiliana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Kwa barua pepe;  gcu@ajira.go.tz au simu 255-687624975
20 Mei, 2013

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger