![]() |
SIKU NASSARI ALIPOTEMBELEWA NA MH WAZIRI MKUU,SELIANI HOSPITALI |
NA SHAABAN MDOE NA LILIAN JOEL,ARUSHA.
UONGOZI wa hospitali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT) ya Selian jijini Arusha umekanusha vikali taarifa zilizotolewa
na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema John Mnyika kuwa serikali ilipeleka
maafisa wa usalama hospitalini hapo kwa lengo la kumdhuru mbunge wa jimbo la Arumeru
Mashariki Joshua Nassari pamoja na majeruhi wa mabomu waliolazwa katika
hospitali hiyo na kusema ni uzushi mtupu.
Mnyika alisema kufuatia kitendo hicho mbunge Nassari alipiga
kelele (yowe) akiwa katika korido ya wodi namba 14 aliyokua amelazwa ili kuomba
msaada baada ya maafisa hao wa usalama waliokua wamevalia mavazi ya kitabibu na
kubeba vifaa vya kitabibu kumtundikia drip aliyohisi ilikua na lengo la
kumdhuru ambayo aliitoa na kuitupa.
Mnyika alitoa kauli hiyo leo alipokua akizungumza na waandishi
wa habari katika viwanja vya mahakama kuu kanda ya Arusha wakati akisubiri
wabunge wanne wa chama chake pamoja na wafuasi wao waliohusika na mkusanyiko
usio halali katika viwanja vya Soweto jijini Arusha jana
Kwa mujibu wa Mnyika, kufuatia hali hiyo Nassari aliamua
kutoroka usiku wa kuamkia leo na kutokomea pasipojulikana ili kujinusuru maisha
yake na kwamba Chadema baada ya kupata taarifa hiyo imeamua kumtafutia mbunge
huyo hospitali nyingine itakayomtibu kwa gharama za chama hicho.
Pia Mnyika alisema mbali na tukio hilo pia polisi kwa
kushirikiana na madaktari wa hospitali hiyo wamekuwa wakiwaruhusu majeruhi wa
tukio la mlipuko wa bomu kwenda majumbani kwao kabla ya kupata naafuu ikiwa ni
hatua ya kupoteza ushahidi wa tukio hilo.
“Nassari amelazimika kutoroka hospitalini pale jana usiku
baada ya kutundikiwa drip na watu tunaowajua ni maafisa usalama iliyokua na
lengo la kummaliza ambayo aliitoa na kasha kuanza kupiga yowe katika korido ili
kuomba msaada na alifanikiwa kutoroka sasa tutmtibu sisi wenyewe”alisema
Mnyika.
Mnyika aliwataja maofisa usalama hao kuwa John Ngowi na
Flugence Mark ambao wamekuwepo hospitalini hapo kwa siku kadhaa wakitoa huduma
kwa majeruhi wa ajali ya mlipuko wa bomu lililosababisha vifo vya watu nne na
kujeruhi zaidi ya 70.
Akijibu tuhuma hizo Kaimu mganga Mkuu wa hospitali hiyo Paul
Kisanga alisema si kweli kwamba mbunge huyo alitoroka hospitalini hapo bali
alipewa ruhusa katika hali ya kawaida baada ya kuonekana hana tatizo lolote
linalomsumbua tangu kufika hospitalini hapo.
Dk.Kisanga alisema mbunge huyo alipewa ruhusa hiyo siku ya
Jumanne majira ya saa 9.30 alasiri bila kuwa na malalamiko yoyote kuhusu kutaka
kudhuriwa na madaktari anaowadai kuwa ni maafisa usalama waliotumwa na
serikali.
Aidha alisema mbunge huyo katika kuondoka kwake hakua na
masharti yoyote kuwa anahitaji kupata uhamisho wa kwenda katika hospitali
nyingine yoyote kwa matibabu zaidi kwakua hata alipotembelewa na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda alimweleza wazi kuwa afya yake imeimarika.
“mimi namshangaa Nassari kama kweli ametoa tuhuma hizo sisi
tumemruhusu baada ya kusema kuwa anaona afya yake imeimarika na hata mbele ya
waziri mkuu aliyasema hayo na kwanini hakuyasema hayo kwa uongozi wa hospitali
kabla huu ni uzushi”alisema Dk.Kisanga.
Wakati huo huo, Kaimu mganga huyo alisema mototo Fahali
Jamali (7) aliyekua amelazwa katika chumba cha ungalizi maalumu (ICU) tangu siku ya
tukio amefariki dunia jana saa saba mchana kufutia hali yake kuwa mbaya zaidi.
Dk.Kisanga alisema marehemu Fahali alifariki dunia kufuatia
majeraha makubwa kichwani yaliyosababisha matundu matatu aliyoyapata kutokana
na kulipukiwa na bomu siku ya tukio hilo.

Aidha aliongeza kuwa mara baada ya marehemu huyo kufariki
mwili wake ulichukuliwa na jeshi la polisi pamoja na mzazi wake hadi katika hospitali
ya mkoa ya Mount Meru kwaajili ya uchunguzi zaidi kabla ya taratibu za maziko
kufanyika.
kazi nzuri sana mkuu wangu wakazi imependeza zaidi .
ReplyDeletebabu kubwa
ReplyDelete