Friday, June 21, 2013

Nassari ashukuru Naibu Waziri, Mbunge

MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) amekanusha kutoroka hospitalini jijini Arusha na badala yake ameshukuru Naibu Waziri na Mbunge kwa kumhangaikia.


Akizungumza jana katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) alikolazwa baada ya kuhamishiwa hapo kutoka Arusha, Mbunge huyo alisema alipewa rufaa na huduma ya kusafirishwa kwa ndege hadi MOI.

Alimshukuru Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR- Mageuzi) kwa jitihada za kuhangaika pamoja na Ofisi ya Bunge na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kukodi ndege iliyomwezesha kufika hospitalini MOI.

Nassari alisema hayo wakati akiendelea na vipimo vya shingo na uti wa mgongo hospitalini hapo.

“Nawashukuru sana Nyalandu na Mbatia, kwani baada ya kusikia ninaumwa na nimelazwa, amekuwa (Mbatia) akihangaika na kujulisha ofisi za Bunge kuhakikisha ninapewa huduma, ambapo walikodi ndege na kunifikisha hapa,” alisema Nassari.

Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi alisema Nassari anaendelea na vipimo hivyo ambapo jana alitakiwa kufanyiwa kipimo cha MRI kwa ajili ya uti wa mgongo na shingo.

Nassari alisimulia, kwamba aliumizwa zaidi kifuani, kichwani na katika uti wa mgongo, kwani alipigwa sana kwa marungu jambo lililosababisha kutokwa na damu nyingi puani.

Alisema baada ya kufika MOI, alifanyiwa vipimo kikiwamo cha X-ray na kuangalia pingili za mgongo na kukutwa ziko sawa ingawa misuli inayozunguka uti haiko sawa, hivyo kushauriwa kufanya kipimo cha MRI.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, jana alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema Nassari alitoroka kwenye Hospitali ya Rufaa ya Selian, Arusha ambako alikuwa akipatiwa matibabu.


Mnyika alidai, kwamba Mbunge huyo, alifanya hivyo baada ya kupata hofu ya kudhuriwa na maofisa wa usalama aliodai walikuwa wamevalia mavazi ya kidaktari.


Katika mkutano na waandishi wa habari, Mnyika alidai Nassari aliwafahamu maofisa hao kwa majina, ambao walikuwa wakimtafuta wodini bila kufahamu walikuwa na lengo gani.


“Baada ya mbunge wetu kubaini hali hiyo, alipiga yowe ambayo iliamsha wagonjwa waliokuwa wodini na maofisa hao kukimbia na yeye kutumia fursa hiyo kutoroka ili kuokoa maisha yake,” alikaririwa Mnyika.

Hata hivyo, Mganga Msaidizi wa Hospitali hiyo, Dk Paul Kisanga alikaririwa akikanusha taarifa ya Mnyika kwa kusema Nassari alipewa ruhusa baada ya hali yake kuridhisha.

Nassari inadaiwa alipigwa wilayani Monduli kwenye Kata ya Makuyuni siku moja kabla ya uchaguzi wa udiwani kwenye kata hiyo.
By Lucy Lyatuu

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger