Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo(kulia)akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Karatu Mwenge wa Uhuru ukimbizwe wilayani humo |
Sote
tunatambua kwamba kihistoria, mwenge wa Uhuru uliwashwa ili kuleta matumaini
pasipo na matumaini, kuleta upendo palipo na chuki, na heshima pale ambapo
pamejaa dharau. Hadi sasa, pamoja na kuhimiza maendeleo kwa wananchi, Mwenge wa
Uhuru bado unabeba maana na madhumuni yale yale yaliyoainishwa wakati
unawashwa.
Katika
mwaka 2013 Halmashauri ya Jiji la Arusha
imepokea Mwenge wa ishirini na moja (21) tangu Mwenge wa Uhuru
ulipowekwa chini ya utaratibu na usimamizi wa Serikali mwaka 1992.
Mwenge
wa Uhuru katika Jiji la Arusha ulipokelewa
tarehe 07 Juni, 2013 kwenye Kata ya Olasit, eneo la uwanja wa Kiwanda
cha A-Z- Kisongo na ulikimbizwa kwa siku moja katika Tarafa tatu (3) za Themi,
Suye na Elerai. Aidha mwenge ulipita
katika Kata sita (6) kati ya kata kumi na tisa (19) za Wilaya hii. Kata
hizo ni Olasiti, Sombetini, Terrati, Sokoni 1, Engutoto na Sekei. Mbio za
mwenge wa Uhuru za Mwaka 2013 zimekuwa
na urefu wa kilometa 71.25 katika Wilaya ya Arusha.
Jumla
ya miradi 8 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Billioni mbili, millioni mia
nane na mbili laki moja na themanini na
mbili elfu mia saba na saba (2,802,182,707/=) ambayo imegharamiwa na Serikali
Kuu, Wabia wa Maendeleo, Halmashauri, na nguvu za Wananchi imepitiwa na Mwenge.
Miradi minne (4) imefunguliwa, mmoja (1) umezinduliwa na mitatu (3) imewekwa
mawe ya msingi.
Miradi
yote iliyopitiwa na Mwenge imegusa Sekta za Kilimo, Maji, Afya, Ujenzi, Elimu
na Utawala bora.
Aidha,
Mwenge ukiwa Jijini Arusha ulikagua miradi ya Uhifadhi wa Mazingira, masuala ya
kupambana na Rushwa, Ukimwi, Madawa ya kulevya na shughuli za Ujasiriamali kwa
Vijana na Wanawake.
Hakika
miradi hii yote inastahili kufunguliwa
na Mwenge kwa sababu ya umuhimu wake kwa jamii ya wananchi wa Wilaya ya Arusha.
Miradi yote iko katika hatua nzuri na thamani ya fedha inaonekana.
Mkuu
wa Wilaya ya Arusha Mhe. John V.K. Mongella akizungumzia tathmini ya miradi
iliyofunguliwa na Mwenge alisema “ Kupitia miradi yote iliyopitiwa na Mwenge wa
Uhuru 2013, Wilaya yetu imeweza kuandaa fursa ya nafasi kwa wanafunzi
wanaomaliza darasa la Saba waweze kujiunga na masomo ya Sekondari kupitia
Ujenzi wa madarasa, kurahisisha usafiri kwa wananchi katika uboreshaji wa Miundombinu, kuongeza
Upatikanaji wa huduma za Afya kwa Kwa kujenga Zahanati, kusambaza maji safi na
salama kwa wananchi, kuimarisha Usalama wa Raia na kupunguza Uhalifu kwa
kujenga Kituo cha Polisi na Utunzaji wa mazingira.
Aidha
Mkuu wa Wilaya amewashukuru wadau mbalimbali waliohusika kwa namna moja au
nyingine katika kuibua, kuchangia na kufanikisha miradi yote iliyopitiwa na
Mwenge. Pia wananchi wote wa Wilaya ya Arusha waliojitokeza kwa wingi kupokea,
kukimbiza na Kukesha na Mwenge.
Ujumbe
wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu utakimbizwa ukiwa unaelimisha na kueneza
ujumbe wa ‘‘Watanzania ni wamoja’’ chini ya kauli mbiu ‘‘Tusigawanywe kwa
misingi ya tofauti zetu za Dini, Itikadi, Rangi na Rasilimali’’ Aidha ujumbe
huu umeambatana na kauli mbiu ya Miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ni
Ushindi wa Watanzania wote na mapambano dhidi ya UKIMWI, Rushwa na matumizi ya dawa za kulevya.
Mwenge
wa Uhuru mwaka huu uliwashwa tarehe 06 Mei, 2013 huko Mkoa wa Kusini Pemba na
utazimwa tarehe 14 Oktoba, 2013. Mkoani Iringa.
Nteghenjwa
Hosseah
Afisa
Habari
Halmashauri
ya Jiji - Arusha
No comments:
Post a Comment