Thursday, July 11, 2013

MH. LOWASSA AWASEMEA WAZEE

Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje

na Ushirikiano wa Kimataifa (Mb) na

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward Lowassa

amesisitiza haja na umuhimu wa kuwapo

kwa ubia kati ya serikali na sekta binafsi

katika kuzikabili changamoto zinazotokana na

ongezeko kubwa la idadi ya wazee.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa akizungumza wakati wa majadilino yaliyohusu namna ya kuingiza suala la wazee katika ajenda mpya za Maendeleo baada ya mwaka 2015. Mkutano huo ulioambatana na chakula cha mchana ulifanyika siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na ulioandaliwa na United Nations Foundation kwa kushirikiana na Mashirika mengine ya Kimataifa. katika mchango wake, Mhe. Lowassa amesisitiza umuhimu wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi katika kuzikabili changamoto za ongezeko la idadi ya wazee duniani. Inasemekana miaka michache ijayo idadi ya wazee duniani itazidi idadi ya watoto wadogo chini ya miaka mitano. Pamoja na Mhe. Lowassa wengine waliochangia majadiliano hayo ni Bi. Ann Pawliczko kutoka UNFPA wa pili kutoka kushoto, Bw. Jack T. Watters kutoka Pfizer, Bw. Paul Ong HelpAge International, Bw. Sharig Khoja kutoka United Nations Foundation, aliyeketi karibu na Mhe. Lowassa ni Bi. Jane Barratt aliyeratibu majadiliano hayo.
Mhe. Lowassa akipeana mkono na mmoja wa waandaji wa majadiliano hayo kuhusu Wazee, takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu ( UNFPA) zinazonyesha kwamba mwaka 1950 idadi ya wazee duniani waliokuwa na miaka 60 au kuzidi ilikuwa milioni 205, 2012 idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia 810 milioni. Inakadiriwa kwamba idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia Bilioni 1 si zaidi ya miaka kumi ijayo na ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea itafikia bilioni 2. Aidha duniani kote wanawake ndio wanaokadiriwa kuishi umri mrefu zaidi kuliko wanaume.

Sehemu ya washiriki wa majadiliano hayo wakiwamo pia Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa.
Mhe. Edward Lowassa akibadilishana mawazo na Balozi wa Zimbabwe katika Umoja wa Mataifa, Bw. Chitsaka Chipaziwa.
Mh. Lowasa akiwa na mmoja wa washiriki wa majadiliano kuhusu mstakabali wa wazee.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward Lowassa ( Mb) amesisitiza haja na umuhimu wa kuwapo kwa ubia kati ya serikali na sekta binafsi katika kuzikabili changamoto zinazotokana na ongezeko kubwa la idadi ya wazee.

“ Maisha Zaidi ya miaka 60 hayapashwi kuwa ya utegemezi, unyonge, kutojiweza au kutokuwa na matumaini. Wazee bado na wanao mchango mkubwa ndani ya jumuiya, jamii, na familia zao ili mradi tu wawezeshwe”.

Na kwa sababu hiyo anasema Mhe, Lowassa, juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea Tanzania ikiwamo za utoaji wa huduma za msingi kama vile Afya , pensheni na uwezeshwaji zinapashwa kuchagizwa na sekta binafsi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa(Mb ), ameyasema hayo siku ya jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wakati aliposhiriki majadiliano kuhusu namna gani suala la Wazee linavyoweza kuingizwa katika ajenda za maendeleo baada ya mwaka 2015.

Majadiliano hayo yaliandaliwa na United Nations Foundation kwa ubia na International Federation of Ageing, Help Age International, AARP, Global Coalition on Aging, mHealth Alliance na Pfizer

“Kama kundi hili la wazee likiwezeshwa na kusaidiwa ipasavyo , linaweza kuipatia jamii soko jipya, ujasiriamali, utoaji wa maamuzi, utoaji wa huduma na utalaamu anuai katika maeneo ya sayansi, teknolojia na upatanishi” anasema Lowassa.

Na kuongeza, ili hayo yote na mengine mengi yaweze kufanikiwa panahitajika bajeti ya kutosha kwa ajili ya kundi hilo la jamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya pensheni, huduma za afya ambazo zitakidhi mahitaji ya wazee, huduma za kisaikolojia na huduma za ulinzi jamii.

Hata hivyo anasema, inasikitisha kwamba, katika nchi nyingi za Afrika na nyinginezo hata zile zilizoendelea bado haziwezi kutoa huduma za uhakika na zenye viwango vya kukidhi mahitajio ya wazee.

“Mara nyingi huduma kwaajili ya wazee inabidi zishindane na huduma za makundi mengine kama vile ongezeko la vijana wasiokuwa na ajira, upunguzaji wa vifo vya watoto wachanga na wanawake wajawazito. Hata hivyo pamoja na changamoto zote hizi za vipaumbele hatuwezi kuendelea na utaratibu huu wa kuchagua. Lazima tutumie maandalizi ya ajenda za maendeleo baada ya 2015 kuwahudumia wazee” anasisitiza Lowassa.

Akasema Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa kujikumbusha na kujifunza kwa kosa la kutoingiza suala la Wazee katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) yanayoelekea ukingoni, kwa kuhakikisha kwamba Wazee wanaingizwa katika malengo mapya ya maendeleo baada ya 2015 kwa kuwa ni suala ambalo haliepukiki.

Akizungumzia hatua mbalimbali zinazochuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwahudumia wazee, Mhe. Lowassa anasema kama ilivyo kwa nchi nyingine, Tanzania nayo inakabiliwa na ongezeko la idadi ya wazee.

Kwa mfano, amesema asilimia 4.5 ya idadi ya watu, ni watu walio na umri wa miaka 65 wastani wa juu zaidi kuliko ule wa asilimia 3.6 Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“ Asilimia 80 ya watu hawa wanaishi vijijini na maisha yao yanategemea kilimo. Serikali inajitahidi kadri iwezavyo kutoa huduma za msingi kwa kundi hilo ingawa pia, na kama ilivyo kwa nchi nyingine, tunakabiliwa na changamoto nyingi kukidhi mahitaji yote ya wazee”. Akabainisha.

Akatumia pia fursa hiyo kuyashukuru mashirika ya kimataifa kama vile Help Age International ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake nchi nchi tangu mwaka 1993.

Akatoa mfano kwa kusema Shirika hilo, mwezi Juni mwaka huu kwa kushirikia na Pfizer limezindua mpango wa miaka miwili wa kupunguza athari zitokanazo na magonjwa yasiyoambukiza (NCD) ambayo yamekuwa yakiwaathiri wazee.

Akasema utoaji wa huduma hiyo unakwenda sambamba na juhudi za serikali katika kukabiliana na magonjwa hayo.

Akatoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano huo na kwamba serikali itakuwa tayari kushirikiano nayo,Takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu ( UNFPA) zinaonyesha kwamba, katika kila sekunde watu wawili duniani wanaadhimisha miaka 60 ya kuzaliwa kwao, na kwa mwaka karibu watu milioni 58 wanaadhimisha miaka 60 ya kuzaliwa.

Aidha katika kila watu nane, mmoja ana miaka 60 au zaidi na makadirio yanaonyesha kwamba ifikapo mwaka 2050 katika kila watu watano mmoja atakuwa na miaka 60 au zaidi.

Ongezeko la idadi ya wazee duniani linachangiwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na ongezeko la umri wa kuishi ambapo katika nchi 33 raia wao wanaishi zaidi ya miaka 80 wakati miaka mitano iliyopita nchi ambazo umri wa kuishi ulifika miaka 80 zilikuwa 19 tu. Utafiti zaidi unaonyesha , umri wa kuishi utaongezea hadi kufikia miaka 90 au hata miaka 100. Japani kwa sasa ndiyo inasemekana kuongoza kwa kuwa na asilimia 30 ya wazee lakini ifikipo mwaka 2050 nchi 64 zitaungana na Japani kwa kuwa na asilimia 30 au zaidi ya wazee.

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger