Thursday, January 24, 2013

Serikali kulipa mamilioni wakazi wa Kigamboni

Mwandishi wetu Joseph Mabula   

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametangaza neema kwa wakazi wa Kigamboni ambako mradi wa uendelezaji wa mji mpya utafanyika na kwamba katika eneo hilo, hoteli zenye hadhi ya nyota tano na vyuo vikuu vitajengwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Profesa Tibaijuka, alisema wakazi ambao nyumba na maeneo yao yatakuwemo katika mradi huo utakaokuwa na nyumba zaidi ya 20,900, hawatahamishwa na badala yake watapatiwa nyumba zenye thamani ya fidia watakayopewa.

Prof. Tibaijuka alisema mfidiwa atakuwa na fursa ya kuchagua thamani ya nyumba anayoitaka kulingana na fidia yake na kusisitiza kuwa kutakuwa na benki zinazotoa mikopo kwa wale wanaohitaji.
KIGAMBONI

“Mfano ikiwa thamani ya nyumba ya mfidiwa ni sh. milioni 100 na yeye anahitaji nyumba ya sh. milioni 120, atatakiwa kupata mkopo kutoka benki, lakini ikiwa atachukua nyumba yenye thamani ya chini, fedha itakayosalia atatumia kwa mahitaji mengine,” alisema Prof. Tibaijuka.

Alisema mradi huo utasimamiwa na wakala maalumu aliyemtaja kwa jina la Kigamboni Development Agency (KDA). Waziri alisema wakala huyo aliteuliwa na Serikali Januari 8, mwaka huu, kusimamia uendelezaji wa mji huo kama mamlaka ya upangaji wa mji.

Prof. Tibaijuka alisema eneo litakalosimamiwa na KDA, lina ukubwa wa hekta 50, 934 na litahusisha kata za Kigamboni, Tungi, Vijibweni, Mjimwema, Kibada Somangila, Kisarawe II, Kimbiji na Pemba Mnazi.

Waziri alisema kuwa uendelezaji wa mradi wa mji mpya utagharamiwa na serikali pamoja na sekta binafsi.   Pia alibainisha kuwa, mbinu za kisasa za kupata fedha ikiwamo kuuza hisa na kutoa hati fungani zitatumika huku akiwataka wawekezaji wa ndani wenye uwezo wa kufanya hivyo, kujitokeza ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa na kuwa kitovu cha kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Jiji la Dar es Salaam.

Alisema matokeo ya mradi huo, ni kuwa mji uliopangwa kwa kiwango cha kimataifa ambao utakuwa mfano wa kuigwa na miji mingine nchini sanjari na kupunguza ujenzi holela.

Matokeo mengine ni kufanikisha wananchi wengi kumiliki nyumba katika maeneo yaliyopangwa na kutumia nyumba zao kupata mikopo kwa ajili ya kuinua vipato.

Prof. Tibaijuka alisema ili kufanikisha mradi huo, KDA itakuwa inajitegemea katika utawala wake ikiwa tofauti na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke pamoja na kuwa na baraza lake la madiwani.

Waziri huyo alikanusha wananchi wa Kigamboni kutohusishwa katika mradi huo. Alibaisha kuwa jambo hilo lipo katika sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na jimbo hilo lipo chini ya mbunge chama hicho, hivyo lilipitishwa katika kampeni za uchaguzi uliopita na ikiwa ni moja ya ahadi zilizotolewa na CCM.

No comments:

Post a Comment

 
Support : Katibu Mwenezi CCM (w) Arusha | Jasper Kishumbua | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali Blog - Arusha - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper Kishumbua
Proudly powered by Blogger