MAMLAKA ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) imeandaa mkakati wa kuanzisha kambi za vijana ikiwa ni njia mojawapo ya kuwahamasisha kujishughulisha katika kilimo kupitia Mpango wa Uendelezaji wa Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT)
Mkurugenzi Mkuu wa RUBADA, Aloyce Masanja, alisema hayo wakati wa semina ya kuwajengea uwezo watendaji wa ngazi ya vijiji hadi wilaya wilayani Ludewa, Njombe juu ya mpango mzima SAGCOT na Kilimo Kwanza.
Alisema vijana wengi nchini wamekuwa wapigadebe wakubwa katika siasa bila kujishughulisha na shughuli za maendeleo, hivyo wao kama mamlaka wana wajibu wa kuwajenga kifikra ili waweze kufanya kazi za kilimo na kuweza kuimarisha uchumi wao na familia zao.
Akitolea mfano nchi ya Korea, alisisitiza kuwa Wakorea wamepiga hatua kubwa kwa kujikita katika sekta ya kilimo, hivyo ni vema Watanzania hasa vijana wakaelekeza nguvu zao katika kilimo, ili kuweza kuinua uchumi wa nchi na kuimarisha ustawi wa jamii.
Aliongeza kuwa, Wilaya ya Ludewa ina fursa nyingi za kilimo, hivyo ni wajibu wa kila mwana-Ludewa kujivunia hali hiyo ili waweze kuitumia kwa uhakika katika kukuza kilimo hasa kilimo cha biashara ili kuongeza kipato.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Fidelis Lumato, alisema wilaya hiyo ina eneo lenye ukubwa wa hekta 839,700 na kati ya hizo 207,200 ni eneo lenye maji, hivyo ni ukanda unaofaa kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji.
No comments:
Post a Comment