Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova |
ULINZI umeimarishwa katika mitaa ya Dar es Salaam huku baadhi ya barabara zikifungwa kwa kipindi maalumu kwa ajili ya ziara ya Rais Barack Obama wa Marekani nchini Julai 1 na 2.
Licha ya ujio wa Rais Obama pia Dar es Salaam iko katika heka heka za mapokezi ya marais 14 na wajumbe watakaoshiriki kesho Jukwaa la Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote. Mfalme Mswati wa II wa Swaziland aliwasili jana kwa ajili ya kuhudhuria jukwaa hilo.
Rais wa Sri Lanka, Mahinda Rajapaksa pia atakuwapo; pamoja na kuhudhuria jukwaa hilo, atafanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete na kutembelea Hekalu la Kibudha, Upanga, Dar es Salaam lililojengwa na Sri Lanka miaka 93 iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu ujio wa Obama, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema Jeshi hilo litasambaza askari wake maeneo kadhaa ya jijini ili kuimarisha ulinzi.
“Pia baadhi ya barabara zitafungwa kwa kipindi maalumu, kiongozi huyu atakapokuwa anazitumia, naomba wananchi wasiogope watakapoona askari mitaani, lakini pia tunaomba ushirikiano mwananchi atakapoambiwa asipite sehemu,” alisisitiza Kova.
CUF yazuiwa Kutokana na ugeni huo wa viongozi wakuu wa nchi akiwamo Obama, maandamano ya Chama cha Wananchi (CUF) yaliyokuwa yamepangwa kufanyika keshokutwa yamezuiwa.
Kamanda Kova alisema barua ya kuomba maandamano hayo ilikuwa na kumbukumbu namba CUF/OK/ DSM/KR/KM/003/1A/2013/24. Alisema baada ya kupokea maombi hayo, Jeshi hilo lilitafakari na kufuatilia kwa makini na kuona hayawezekani kufanyika .
“Moja ya sababu zilizofanya tusitishe maandamano ni Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo, hivyo maandamano yao yataingiliana na misafara ya viongozi na wajumbe.
Aidha, alisema kutokana na ziara hizo za kiserikali , Polisi imeona itakuwa vigumu kwa Rais Kikwete kupata muda wa kuyapokea. Pia alisema barabara ambayo ingetumika ni ya Uhuru kuanzia kituo cha mafuta cha Buguruni , hivyo kuingiliana na misafara ya viongozi hao, hivyo kuwa vigumu kuyasimamia.
“Polisi inazuia maandamano hayo kwa nia nzuri,” alisema na kuongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa endapo watalazimisha kuandamana na kama hawataridhika wakate rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mabango, vipeperushi
Alisema pia Polisi imepata taarifa za kuaminika kwamba kipo chama cha siasa na taasisi ambazo zimejiandaa kusambaza vipeperushi au kujitokeza na mabango ghafla barabarani wakati wa ujio wa Obama, kitendo ambacho ni kinyume cha taratibu za usalama.
Waziri Membe Akizungumzia ziara ya Obama, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema maandalizi yamekamilika kutokana na Polisi kuweka ulinzi katika maeneo yote atakayopita kiongozi huyo.
Alisema Obama akiwa nchini atatoa hotuba yake kuhusu mradi wa kuboresha uzalishaji wa umeme katika nchi saba ikiwamo Tanzania pamoja na utekelezaji wa miradi ya Changamoto za Milenia (MCC) nchini.
Membe, katika kuzungumzia ziara hiyo, alisema ujio wa Obama ni ishara kuwa pamoja na udogo na hali ya umasikini wa Tanzania, bado inakubalika na mataifa makubwa.
“Hii inaonesha kuwa juhudi za Rais Kikwete zimeonekana na kutambuliwa na mataifa makubwa, hivi karibuni alikuja Rais wa China, Xi Jinping na sasa Obama,” alisema Membe.
Alisema ukweli unajidhihirisha zaidi kutokana na Rais Kikwete kuwa ni mmoja wa viongozi wachache wa nchi zinazoendelea kuitwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi Nane Tajiri Duniani (G8) uliofanyika London, Uingereza.
“Tunajua kuwa kuna wanasiasa wachache wamekuwa wakibeza juhudi za Serikali katika suala la maendeleo, lakini ukweli unabaki kuwa mataifa makubwa yanajua nini Serikali inafanya,” alisisitiza Membe.
Obama na umeme
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally, alisema kiongozi huyo wakati akitembelea mtambo wa umeme wa Symbion, Ubungo atatoa hotuba itakayojikita katika eneo la Sera ya Marekani kuhusu Umeme Afrika.
Alisema Sera hiyo inagusa nchi saba za Afrika ambazo pamoja na Tanzania ni Kenya, Uganda, Ethiopia, Ghana, Nigeria na Sudan Kusini.
Aliwataka wafanyabiashara wa ndani wachangamkie fursa hiyo ya ujio wa Obama kwa kuwa atafuatana na timu ya wafanyabiashara wa Marekani wapatao 500 ambapo pia wapo wafanyabiashara walioalikwa kutoka nchi za Afrika kwenye mkutano wake na wafanyabiashara wa nchini.
Akiwa Senegal Wakazi wa kisiwa kidogo cha Goree, chenye miamba na kumbukumbu mbalimbali za kikoloni -baadhi yao wanaamini kwamba mizimu ya watumwa wa Kiafrika ilipata kushikiliwa mateka hapo-kimekuwa kikitembelewa na viongozi wa dunia.
Obama ambaye alitarajiwa kuwasili kisiwani humo jana, anakuwa Rais wa Tatu wa Marekani kufika hapo akitanguliwa na Bill Clinton na George W. Bush.
Wakazi wa Goree na wa mji mkuu wa Senegal wa Dakar, umbali wa kilometa tatu bara, bado wanazungumzia ziara ya Rais Bush.
Rais huyo wa zamani aliwashangaza wengi kwa hotuba yake juu ya mateso waliyopata watumwa wa Kiafrika katika kisiwa hicho chenye urefu wa kilometa moja, kabla ya kufungwa minyororo na kupakiwa kwenye meli ambazo zilivuka kwenda Marekani.
“Kwa miaka 250 watumwa walipokwa utamaduni na heshima yao,” Bush alisema akiita biashara ya utumwa “moja ya uhalifu mkubwa katika historia.” Lakini si hotuba ya Bush peke yake – aliyotoa wakati huo kwa dakika 20 – kwamba ndiyo wakazi wa hapo wanaikumbuka.
“Wakazi wa Goree bado wanazungumzia ziara ya Bush, na bado wana hasira dhidi yake ,” alisema Sophie Ly Sow, mkazi wa Dakar. “Walizuiwa majumbani mwao, walipigwa marufuku hata kusimama kwenye roshani zao kumtazama. Waliteseka na hali hiyo, lakini hawakupata chochote cha maana.”
Jiji la Dakar lilifungwa kwa siku kadhaa kabla ya ujio wa Bush wana usalama wakisambaa katika migahawa na klabu za usiku na mawasiliano ya simu yakiwa hayapatikani. Wengi wanasema ujio wa Obama ni historia inayojirudia.
Ni mwenzetu
Lakini Wasenegali wanasema bado wana nia njema na Rais wa Marekani, ambaye Waafrika wengi wanamwona kama fahari kwa kuwa ni mtu wao kutokana na kuwa na asili ya Kenya.
Akiwa Senegal, Obama atafanya mazungumzo na Rais Macky Sall, na kukutana na viongozi wa sheria kutoka eneo hilo la Afrika Magharibi, kujadili umuhimu wa utawala wa sheria.
Pia atahudhuria matukio ya usalama wa chakula, kuimarisha sekta ya kilimo na kukuza sekta binafsi. “Senegal … ni mbia mkubwa wa Marekani katika demokrasia,” alisema Ben Rhodes, Naibu Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Ikulu ya White House.
“Tunaguswa sana na jinsi makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani yanavyofanyika kama tulivyoshuhudia katika nchi kama Senegal … na maendeleo makubwa ya kidemokrasia ambayo tunayaona barani kote.
Habari hii imeandikwa na Hellen Mlacky, Halima Mlacha na Mashirika
No comments:
Post a Comment