KAMANDA MBOWE AKIKIMBIA KWENYE ENEO LA MKUTANO UWANJA WA SOWETO |
Chagonja alisema hayo jana mjini hapa akizungumza na waandishi wa habari akisisitiza kuwa kama Mbowe , Lissu na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema hawana imani na Polisi na kuituhumu kuwa mtuhumiwa namba moja wa ml
Alisema lakini litakuwa jambo la kushangaza wabunge hao kukataa kutoa ushahidi Polisi wachunguze tukio hilo lililosababisha vifo vya watu watatu na kupelekea baadhi ya watu kujeruhiwa.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya watu hawapendi kuona Arusha na nchi inakuwa na amani akawasihi Watanzania kutokubali amani iliyopo kuvurugwa na watu wachache. ‘’Natoa mwito kwa viongozi hao watuletee ushahidi huo huku Lema na Mbowe wakijisalimisha Polisi … bado tunashikilia watu watatu ambao hatujawapeleka mahakamani wanaendelea kuhojiwa,” alisema. Alitoa rai kwa wananchi kutokubali kuhudhuria mikutano isiyo na kibali na kuongeza kuwa juzi wabunge wanne wa chama hicho; Lissu (Singida), Mustafa Akonay (Mbulu), Said Arfi (Mpanda Mjini) na wa Viti Maalumu, Joyce Nkya na wafuasi wao 67 walikamatwa na Polisi Soweto kwa kufanya mkutano usio halali na wanafikishwa mahakamani leo.
Chagonja alisema sababu ya polisi kurusha mabomu hayo ni baada ya walinzi wa chama hicho, Red Brigade kumshambulia Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Arusha na mara polisi walipoona OCD anashambuliwa walitumia mabomu kutawanya wabunge hao na wafuasi wao ambao walikusanyika bila kibali.
Alisema polisi walishauriana na Mbowe ili azuie wafuasi hao na waondoke uwanjani hapo baada ya wenye uwanja Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC ) kuzuia shughuli za maombolezo viwanjani hapo na kutarajia kuwa Mbowe angewatangazia wafuasi hao watawanyike, lakini hakufanya hivyo na kuendelea na mkutano.
Mmiliki wa bastola Kuhusu bastola iliyookotwa juzi wakati polisi wakirusha mabomu kutawanya wafuasi hao, Chagonja alisema mhusika alijitokeza jana Polisi na kujitambulisha kuwa mkazi wa Daraja Mbili ambaye hakumtaja jina.
Uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa hajailipia kodi silaha hiyo tangu mwaka 2003 hivyo atatozwa faini na taratibu nyingine zitafuata.
Pia Polisi inaendelea kushikilia magari sita, pikipiki 106 na baiskeli 16 za wafuasi wa chama hicho likiwamo pia gari la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB), Mbowe.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana;
Alisema ni hatari kwa kiongozi mkubwa wa kisiasa kudai ana ushahidi wa tukio hilo, lakini akagoma kuieleza Polisi na akataka kujua uko wapi uzalendo wa kutanguliza maslahi ya Taifa kwa mtu kama huyo.
Akizungumza na gazeti la Habari Leo, jana kwa simu, Dk Bana alisema kila Mtanzania anapaswa kuwa na imani na Jeshi la Polisi kwa kuwa ni chombo cha umma kilichopo kwa mujibu wa Katiba hivyo ni kosa kudai una ushahidi kwa tukio kama lililotokea Arusha lenye sura ya kigaidi, kugoma kuutoa.
Dk Bana alisema hali hii inatia shaka, kwamba ikiwa Chadema wataingia madarakani, wanamaanisha wataunda Polisi yao isiyo na chembe ya Polisi ya sasa na kama sivyo, wanapaswa kuheshimu mamlaka za nchi na sheria zake.
“Jeshi la Polisi lipewe ushirikiano, hasa katika matukio kama haya ya kuudhi, jinai, ugaidi na machafu kwa amani ya nchi yetu, kiongozi kama wa Chadema kudai ana ushahidi lakini hataki kuutoa Polisi, huyu anataka kusaidia kweli nchi yake?,” alihoji Dk Bana. Kutokana na kurushiana maneno kunakoendelea hivi sasa baina ya Chadema na CCM baada ya tukio hilo, Dk Bana alishauri, kwamba huu ni wakati wa vyama hivyo viwili, kukutana na kuzungumza kwa kina kwa usalama wa nchi.
“Natarajia huu ndio wakati wa Chadema na CCM kusahau tofauti zao, nilitarajia yanapotokea mambo kama haya, wangeomba hata kuonana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu kama walivyofanya baada ya uchaguzi, badala yake wanarushiana maneno, hii haijengi, wakutane wazungumze,” alisisitiza Dk Bana.
Alitoa mwito kwa asasi za kiraia, vyombo vya habari, viongozi wa dini na kijamii, wanaharakati, kujitokeza kwa wingi wakati huu, kukemea haya yanayotokea na kushinikiza wanaosema wana ushahidi wautoe ili kuokoa amani ya nchi inayotaka kuharibiwa na wachache.
“Watanzania hatujajengwa katika mazingira ya kurushiana mabomu, haya ni mambo ya kuchukiza na yanatia hasira, watu wanakufa, leo tunasikia Arusha lakini kesho itahamia Dar es Salaam na kwingineko, kutokuwa na uchungu wa kusaidia nchi ni kukosa weledi.
“Siungi mkono kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye wala ya Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe mara baada ya tukio hili, wanarushiana mpira wakati maisha ya Watanzania yanateketea, wakutane kunusuru nchi na watoe ushirikiano kwa vyombo vya Dola,” alisema Dk Bana.
Serikali itulie Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Issa Shivji, aliitaka Serikali kuwa tulivu katika kushughulikia matukio ya kigaidi yanayotokea nchini na kuweka nguvu kubwa kutafuta wahusika badala ya kutumia nguvu hiyo kupambana na vyama vya siasa na wananchi.
Profesa Shivji
Profesa Shivji alisema matukio hayo yana kila dalili ya chokochoko za chini kwa chini zinazofanywa kwa mgongo wa watu wachache kupitia vyama vya siasa, yenye lengo la kuleta machafuko kwa maslahi ya wachache.
Alikuwa akizungumza na gazeti hili juu ya malumbano ya kisiasa baina ya CCM na Chadema yanayoendelea hivi sasa baada ya mlipuko wa pili wa bomu kutokea Arusha. Alisema:
“Binafsi naona hapa wanachanganyana tu, vyama vya siasa vinawachanganya watu na pia vinaichanganya Dola, wanajua ukweli, lakini hawataki kusema, upinzani wanadai wana ushahidi, sasa kwa nini wasifuatwe kwa utaratibu kueleza ushahidi wao?” Alihoji Profesa Shivji.
Aliishauri Serikali kutumia kila namna kuhakikisha inatulia katika kushughulikia matukio haya, la sivyo kuna chokochoko zinazofanywa chini kwa chini, zenye lengo la kuamsha machafuko nchini kwa maslahi ya wachache.
Profesa Shivji anaamini kuna watu nyuma ya matukio haya, wanaojua ukweli halisi wa nini kinaendelea na kuitaka Serikali ambayo anaamini ina Dola yenye nguvu na uwezo wa kumpata mhusika, kujikita kutafuta chanzo badala ya kushughulika na mambo yasiyo na msaada kujua ukweli wa mambo.
Alitumia fursa hiyo, kuomba viongozi wa dini na wasio na dini, kuongeza juhudi kuomba amani ya nchi kwa kuwa, hali ilivyo sasa, watu wanajenga uadui kwa misingi ya vyama vya siasa wakati tatizo ni kubwa zaidi ya vyama hivyo. Mkazi wa Dar es Salaam, Jacob Malihoja katika maoni yake, alisema
“Tusinyoosheana vidole tutakosa nafasi ya kumjua mbaya wetu. Tuwe watulivu, wenye hekima ili Serikali ipate muda wa kulishughulikia. Vinginevyo tutafarakana, tutavuragana na Serikali itajikita kwenye mifarakano badala ya kutafuta mbaya wetu.”
Malihoja katika maoni kwa Gazeti hili, aliendelea kusema, “tukumbuke Tanzania tumeanza kujizolea maadui wanaotokana na wivu wa amani iliyopo. Wapo maadui wanaotokana na mafanikio ya maendeleo ya Taifa na kukubalika na mataifa makubwa.”
Alitolea mfano kwamba ujio wa viongozi wa kimataifa, akiwamo Rais wa China, Xi Jinping na hata matarajio ya ujio wa Rais wa Marekani, Obama, havipaswi kupuuzwa vinaweza kuwa chanzo cha chuki dhidi ya Taifa.
By Veronica Mheta, Arusha
No comments:
Post a Comment